Mshauri wa
Benchi la Ufundi la Taifa Stars, Abdallah Kibadeni ambaye kitaaluma ni kocha,
ametaja sababu ya wachezaji wa Klabu ya Simba kutopata nafasi kubwa katika
kikosi cha kwanza cha Stars katika mechi dhidi ya Nigeria.
Kibadeni
amejitokeza kufunguka juu ya suala hilo ambalo limekuwa likizungumzwa mitaani
kutokana na kikosi cha Stars kukosa mchezaji wa Simba katika 11 walioanza
kwenye mchezo huo wa Jumamosi iliyopita.
Kibadeni ambaye ni gwiji wa Simba amesema
hawakupanga kikosi kwa kuangalia majina ya timu, bali uwezo wa mchezaji na aina
ya mbinu walizozipanga.
“Tulitumia
akili ya kisayansi kukipanga kikosi hicho kutokana na kutojua falsafa na mbinu
za kocha mkuu mpya wa Nigeria, Sunday Oliseh. Tuliamua kuwapanga kutokana na
jinsi walivyozoeana kwa muda mrefu, mfano Barthez (Ally Mustapha), Cannavaro
(Nadir Haroub), Yondani (Kelvin) na Haji Mwinyi wamekuwa wakicheza pamoja na
kwa kuelewana.
“Viungo
Himid (Mao), Mudathir (Yahya), Farid (Mussa) na beki wa pembeni Kapombe
(Shomari) nao wamekuwa na maelewano mazuri kuanzia ngazi ya klabu na hata
tulivyokuwa kambini.
“Katika
safu ya ushambuliaji Samatta (Mbwana), Ulimwengu (Thomas) wote wapo TP Mazembe
wanajuana vizuri. Tulimuongeza Ngassa (Mrisho) kwa kuwa ni mzoefu na uwezo wake
unajulikana.
“Hivyo
hakukuwa na lengo baya kwa wachezaji wa Simba na wala hawatakiwi kulalamika,
ndiyo maana uliona alivyoingia Ndemla (Said) naye alicheza vizuri kwa kuwa
alikuwa ameshausoma mchezo. Tuache lawana na tuwapongeze vijana kwa kazi
nzuri,” alisema Kibadeni.







0 COMMENTS:
Post a Comment