![]() |
| UWANJA WA NYAMAGANA KWA SASA... |
Licha ya
Uwanja wa Nyamagana uliopo Mwanza kuwa wa kwanza kufanyiwa marekebisho ikiwemo
kutakiwa kuwekewa nyasi bandia, wakazi wa jiji hilo wamelalamika kukwama kwa
mchakato huo na badala yake, Uwanja wa Kaitaba uliopo mkoani Kagera kuwa kwenye
hatua za mwisho za marekebisho ikiwemo kuwekewa nyasi bandia.
Wakizungumza
na gazeti hili, baadhi ya wadau wa mchezo wa soka, wamelilalamikia Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF) kutokana na hali hiyo wakidai limeutelekeza Uwanja wa
Nyamagana huku ule wa Kaitaba ukipewa kipaumbele.
Akizungumza
juu ya maendeleo ya Uwanja wa Kaitaba, Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa
Kagera (KRFA), Salum Chama aliliambia gazeti hili kuwa ndani ya wiki tatu
zijazo wanatarajiwa kuona uwanja wao ukiwekewa nyasi bandia baada ya marekebisho
mengine kukamilika.
“Nyasi
zitawekwa hivi karibuni,” alisema kiongozi huyo ambaye chama chake kinaongozwa
na mwenyekiti Jamal Malinzi ambaye pia ni rais wa TFF.
Kuhusu
nyasi bandia, Chama alisema: “Aliyepewa tenda ya kutengeneza uwanja ndiye
ambaye amejitolea kulipia nyasi bandia kutoka bandari, ndiyo maana
zimeshapatikana.”
Akizungumzia
kukwama kwa Uwanja wa Nyamagana, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa,
alisema: “Serikali haijatoa msamaha wa kodi katika vifaa vilivyokwama bandarini
ikiwemo nyasi bandia. Fifa imetuambia kuwa, ikifika Desemba, mwaka huu kama
mambo yatakuwa bado, basi Fifa itazuia miradi yote. Tunasikitika sana kuona
serikali imetugeuka na kukataa kutuondolea kodi kwenye vifaa hivyo.”
Licha ya
kuanza kufanyiwa marekebisho, Uwanja wa Nyamagana umeanza kuchakaa kwa kuwa
matengenezo yamesimama na hakuna kinachoendelea.









0 COMMENTS:
Post a Comment