September 11, 2015


Na Saleh Ally
SIKU ikifikia Kocha Charles Boniface Mkwasa akashindwa kuipa matokeo timu ya taifa, Taifa Stars, basi bila ya kuchelewa wala woga, nitasema, aachie nafasi.


Lakini sasa ni wakati mwafaka wa kusema maslahi yake yaangaliwe ili kwa wakati mwingine tuangalie kama kocha mzalendo na wenzake wazalendo wanaweza kuisaidia timu yetu ya taifa.

Makocha wageni waliopita, walikuwa wakilipwa mshahara zaidi ya Sh milioni 10 kwa mwezi. Aliyeondoka alifikisha hadi Sh milioni 20, lakini hakuwa na lolote.

Hakuna anayeweza kukataa kwamba Kocha Mart Nooij hakuwa na msaada katika kikosi cha Stars, alikuwa tatizo na alichangia kuirudisha nyuma kwa kiasi kikubwa.

Nimekuwa nikisisitiza hili, kwamba TFF ilifanya makosa kumuondoa Kim Poulsen na kumchukua Nooij ambaye huenda alibebwa na urafiki wake na baadhi ya watu wa TFF au ni siasa za soka kwa kuwa uongozi mpya ulitaka usafishe kila kitu kilichokuwa chini ya uongozi uliopita.

Uamuzi wa TFF kwa kipindi hiki kujaribu kumtumia mzawa na hasa Mkwasa, hakika umekuwa ni katika wakati mwafaka na kinachotakiwa ni kuuongezea nguvu kwa kuwaongezea maslahi wahusika.


TFF ilimpa Mkwasa mkataba mfupi wa miezi mitatu kutaka kuiona kazi yake. Hakika kila mtu sasa hana wasiwasi, kwa kile ambacho Mkwasa amekionyesha katika mechi zake mbili.

Wakati Stars ilitwangwa nyumbani mabao matatu na Uganda chini ya Nooij, ikiwa chini ya Mkwasa ilisafiri kwenda Kampala na kutoka sare ya bao 1-1. Ingawa tulitolewa kuwania Chan, tofauti ilionekana.

Mechi iliyofuata ya kuwania kucheza Afcon dhidi ya Nigeria, hakukuwa na matumaini hata kidogo baada ya kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Misri, Stars ikiwa ugenini.

Nani alikuwa na matumaini hata ya sare dhidi ya Nigeria? Nani alikuwa anahisi kuwa Stars itapata hata pointi moja tu katika mechi zake za Kundi G kuwania kucheza Afcon? Matumaini yalishazama.

Sasa Stars inaanza kuinuka angalau kwa sare dhidi ya Nigeria. Lakini kilichowafurahisha Watanzania wengi ni soka safi, soka la kasi, kazi na kushambulia muda wote. Kumbe Mkwasa anaweza?
KIKOSI CHA TAIFA STARS

Yeye kwa kushirikiana na benchi lake la ufundi, wamefanya kazi kubwa. Mimi sizungumzii kishabiki, ndiyo maana nimeanza kwa kusema, siku Mkwasa akikwama, basi nitakuwa wa kwanza kumuomba aachie nafasi hiyo ya Stars.

Kwa sasa, Mkwasa na benchi lake la ufundi, yaani wasaidizi wake, pia mshauri wa ufundi, Abdallah Kibadeni, wanastahili maslahi mazuri.

Nimeishi nao Uturuki wakati Taifa Stars ikiwa kambini. Walionyesha kiasi gani walivyokuwa na juhudi kubwa kutaka kuisaidia timu na kufanikisha kazi yao. Walionyesha kiasi gani walivyokuwa na hofu ya kufeli, walijua wataambiwa wamefeli kwa kuwa ni wazalendo, hivyo juhudi ya kutaka mafanikio ilikuwa kubwa sana.

Sasa ndiyo wakati mwafaka, iwahiwe kabla haijafa na kuwapatia maslahi bora ili waiendeleze ili kuinua morali na heshima ya soka nchini ambayo sasa ni matope kabisa.

Mshahara aliokuwa analipwa Nooij kutoka kwa Rais Kikwete uko wapi? Vipi Mkwasa aliyeonyesha matumaini na sasa anafanya vizuri asipewe, wakati Nooij aliyeboronga alikuwa akipewa?

Sitaki kuamini kwamba kwa kuwa ni Mzungu, kwa kuwa ni mgeni basi inawezekana akalipwa vizuri zaidi hata kama anavurunda, halafu mzalendo halipwi vizuri hata kama anafanya vizuri.
Miezi mitatu aliyopewa na TFF imepita, kaiongoza timu katika mechi mbili na mambo yameenda poa kabisa. Sasa ni wakati wa kumlipa mshahara ili ikiwezekana aachie kazi yake Yanga na kuwekeza nguvu zake zote katika kikosi cha taifa.

Ninaamini Rais Kikwete atasoma makala haya na kulifanyia kazi hili kwamba asiondoke mwezi ujao kabla mshahara haujamfikia Mkwasa, chonde.

Hakuna sababu ya sisi watu wa soka kuanza kuandika mabango “Rais Kikwete, Mkwasa unamuachaje?” Namuomba aupitishe mshahara ufike kwa Mkwasa ambaye sasa anastahili kuupata.

Rais Kikwete hana tatizo, watu wa wizarani kama wanataka kuleta figisu, basi huu si wakati wake na wanapaswa kujali uzalendo na thamani ya kazi.

Kama ukivunja morali aliyonayo Mkwasa kwa kipindi hiki ni rahisi sana kuvunja morali ya wengi katika timu hiyo. Chonde Rais Kikwete, mpe Mkwasa mshahara wake ili kazi iendelee vizuri.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic