CHAMA cha Waandishi
wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kitatoa tuzo kwa Rais Jakaya Kikwete
pamoja na wanamichezo 10 waliofanya vizuri zaidi katika miaka 10 akiwa Rais wa
Tanzania.
Tukio hilo ambalo pia
litahudhuriwa na Rais Kikwete, litafanyika Oktoba 8, mwaka huu ukumbi wa
Mlimani City, Dar es Salaam likiwa na lengo la wanamichezo kumuaga Rais Jakaya
Kikwete.
TASWA itakabidhi tuzo
maalum kwa Rais ikiwa ni kuthamini mchango wake kwa maendeleo ya michezo wakati
wa miaka 10 ya uongozi wake na imebariki tukio hilo kama ‘JK na
Wanamichezo’.
Licha ya kutoa tuzo kwa
Rais na wanamichezo 10 waliofanya vizuri zaidi, pia TASWA itatoa vyeti maalum
kwa kampuni mbalimbali zilizosaidia kwa kiasi kikubwa kudhamini michezo katika
miaka 10 ya Rais Kikwete.
Maandalizi muhimu
yamekamilika kuhusiana na tukio hilo, ambapo wawakilishi kutoka vyama vyote vya
michezo hapa nchini pamoja na wanamichezo wataalikwa kuhudhuria tukio hilo la
kihistoria.
TASWA inamshukuru Rais
Kikwete kwa kukubali kujumuika nasi siku hiyo ili kuagana na wanamichezo, ambao
wameshuhudia mambo mazuri akiwafanyia katika uongozi wake, ambao utafikia
tamati baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba
25, mwaka huu.
Pia TASWA inaishukuru
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa ushirikiano mkubwa iliotoa
kuhakikisha tukio hilo linafanikiwa.
Tayari wadhamini
mbalimbali wamejitokeza kusaidia na tunaomba wengine watuunge mkono, ambapo
Jumanne Oktoba 15, TASWA itafanya mkutano na waandishi wa habari kutangaza
mdhamini mshiriki mmoja, mkutano utakaofanyika ukumbi wa City Sports Lounge,
Dar es Salaam.
TASWA imeona kuna haja ya wanamichezo kuagana na Rais Kikwete na kumpa tuzo kutokana na
masuala mbalimbali aliyofanya kwa miaka yake 10 katika kusaidia kukuza michezo
na sanaa hapa nchini.
Baadhi ya mambo hayo ni serikali yake
ilivyolipia makocha wa michezo ya soka, netiboli na ngumi na pia
serikali ilipeleka wanariadha wetu China, Ethiopia na New Zealand kwa
maandalizi ya mashindano ya kimataifa.
Pia tutamkumbuka Rais
Kikwete kwa uamuzi wa kurejesha michezo shuleni pamoja na mashindano ya michezo
kwa shule za msingi na sekondari (UMISHUMTA na UMISETA).
Yapo mambo mengi ambayo
tukiyataja yote aliyofanya kuhusu michezo yatachukua nafasi kubwa, hivyo tuna
kila sababu wanamichezo kujitokeza na kuagana na Rais wetu.
Ahsanteni,
Juma Pinto
Mwenyekitii TASWA
11/09/2015.








0 COMMENTS:
Post a Comment