Na Saleh Ally
WAKATI tunaanza safari na kikosi cha Taifa
Stars kwenda nchini Uturuki kwa ajili ya kambi ya siku nane, nilianza kuona
mambo mengi sana tofauti ambayo mwisho yamekuwa na faida na huenda ikawa kubwa
kama hatari nitakazozielezea zitaepukwa.
Nimesafiri na timu mbalimbali kwa zaidi ya
miaka 15, zikienda kucheza mechi nje ya nchi. Tofauti kubwa niliyoiona na Taifa
Stars katika safari ya Uturuki, kuanzia wachezaji, meneja, mshauri wa ufundi,
kocha msaidizi na kocha mkuu pia viongozi wote hadi msemaji wa shirikisho na
waandishi wote walikuwa ni Watanzania.
Kuwepo kwa Watanzania tupu katika kikosi
hicho, hali ya upendo na uzalendo ilikuwa juu sana na ilionekana wengi walikuwa
ni watu wanaoelewana na wenye lengo moja.
Utanzania wa pamoja na hasa mnapokuwa mbali,
unajenga uzalendo unaotokea moyoni na lengo la kutaka kufanya vizuri. Unaweza
kusema kwamba kila kitu kimeonekana katika mechi dhidi ya Nigeria, taifa kubwa
kisoka Afrika.
Nigeria wameponea chupuchupu katika mechi
hiyo ya kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya Taifa Stars
na hakuna anayeweza kubisha tena kwamba kikosi cha Tanzania ndiyo
kilichoonyesha soka safi zaidi, lakini kikashindwa kutumbukiza tu mpira wavuni.
Hapa kuna mengi ya kujifunza, kama kweli
makocha wazalendo wataaminiwa basi wanaweza kutufikisha mbali lakini lazima
wawe na mwenendo wa Mkwasa na msaidizi wake, Hemed Morocco pia mshauri wa
ufundi, Abdallah Kibadeni ambao wanaonyesha ni watu wanaotaka kufanikiwa.
Baada ya mechi ya jana ya Taifa Stars,
hakuna ubishi sasa gumzo ni uwezo waliouonyesha Taifa Stars kwani kwa kiwango
kikubwa unazidi ule wa makocha waliopita, hasa wageni kutoka Ulaya na
kwingineko.
Mara ya mwisho kocha mzalendo alikuwa ni
Mshindo Msolla, akachukua Marcio Maximo takriban miaka kumi iliyopita. Baada ya
hapo Wazungu walikuwa wakipokezana kikosi kama pasi za samba za Brazil.
Aliyepita Mart Nooij ndiye alikuwa ‘matope’
kabisa kikazi na kujisifia kwake ni uwezo mkubwa wa kunywa bia tu. Tunajua
kwamba uongozi mpya wa TFF ulikurupuka na kumchukua kwa kuwa ulitaka kubadili
kila ulichokikuta. Lakini sasa unaweza kuwapongeza, wameona kosa na kufanya
kilicho sahihi.
Baada ya kiwango kizuri katika mechi hiyo
dhidi ya Nigeria sasa hakuna ubishi, kuanzia mashabiki na vyombo vya habari
tutasifia kwa kuwa ndiyo hali halisi.
Kusifia hakukwepeki, lakini tusipoangalia
inaweza ndiyo ikawa hatari ya baadaye kwani kama wanaosifiwa watashindwa
kujitambua, basi mwisho wa kiwango bora kama hicho unaweza ukawa ni katika
mechi hiyo tu, basi.
Asilimia 85 ya wachezaji wa kikosi cha Taifa
Stars ni makinda, asilimia 90 ni wanaocheza soka nyumbani. Lazima wawe imara
kujua mambo mengi ya msingi ili kuepuka kuyumba.
Kwanza wanaposifiwa, ukomo wa sifa unabaki
kuwa kwenye ‘kontrol’ yao wenyewe. Kwamba sifa hizo zisiwaleweshe hadi
wakafikia kusahau majukumu yao watakaporejea katika klabu zao.
Kikosi cha Taifa Stars kinapendeza kikibaki
hichohicho lakini kitakuwa hivyo kama wachezaji hao watarejea katika klabu zao
na kufanya vizuri ili Mkwasa aweze kuwaita tena. Lakini wakirudi wamelewa sifa,
maana yake hawatarudi na kusababisha kuwa na kikosi kinachobadilika kila mara.
Mkwasa atapenda kuendelea na kikosi hicho,
lakini kamwe hawezi kumchagua mchezaji ambaye anakaa benchi katika klabu. Kupata
namba ni kazi ya mchezaji mwenyewe.
Si arudi katika klabu yake, abweteke kwa
kuwa alifanya vizuri katika mechi dhidi ya Nigeria, maana yake atakaa benchi na
Mkwasa hatamuita.
Wapo ambao wamekuwa wakilaumu vyombo vya
habari kwamba vinawaharibu wachezaji kutokana na kusifiwa. Basi wachezaji wa
Tanzania wangekuwa wanaishi Uingereza, wangekufa kwa sifa ambako wanawasifia
kweli na wakikosea, wanawaponda vibaya.
Hapa Tanzania wanasifiwa kidogo tu, hata
‘kutandikwa’ ni kidogo tu. Vyombo vya habari viachwe vifanye kazi yake hasa
kama ina uhalisia, mchezaji ajitambue naye afanye kazi yake na hiyo ndiyo hali
halisi.
Kama mchezaji atalewa sifa kutokana na
kusifiwa na vyombo vya habari, hilo ni tatizo lake kubwa, ndiyo maana
nawashauri kujitambua na kuacha kuyumbishwa na sifa.
Mashabiki nao wanahusika kuitengenezea Taifa
Stars hatari. Kuna rekodi nyingi kupitia klabu hasa kongwe za Yanga na Simba,
wapo mashabiki wanaoona sifa kubwa kuwanunulia wachezaji vilevi au kuwatafutia
wanawake wazuri kama zawadi ya kufanya kazi yao.
Fitness waliyokuwa nayo Taifa Stars baada ya
kambi ya Uturuki imekuwa msaada mkubwa sana. Lazima itunzwe, wachezaji lazima
wajue adui yao siyo sifa za vyombo vya habari, badala yake kutojitambua na
anasa.
Lazima wayatunze mazoezi, lazima wajitunze
wao wenyewe ili kufanya kiwango kibaki kuwa juu na ikiwezekana kipande. Kama
watakishusha, hakika hata Mkwasa watamuangusha.
Taifa Stars haiwezi kwenda Uturuki kila
kabla ya mechi, TFF haiwezi kuhimili gharama, ndiyo maana nilishangazwa kusikia
watu wakilazimisha mashabiki waingie bure! Hivyo mazoezi waliyoyapata Uturuki
yatunzwe na lazima wajue kuyapata tena ni gharama kubwa.
Ruksa wayatumie katika klabu zao, lakini
mwisho tena yawe na faida kwa Taifa Stars. Suala la anasa liwe sumu kwao ili
kuepusha hatari ya Taifa Stars kuwa kikosi kinachobadilika hovyo au kutumia
wachezaji wenye kiwango cha ‘tiamaji tiamaji’!
Walichokifanya Taifa Stars ni kitu safi
sana, kujipongeza angalau kidogo si vibaya. Lakini lazima wajitambue na wao
ndiyo wanabaki wenye nafasi ya kuendeleza kilichoanza au kukifanya kiwe cha
kuyumba kutokana na umakini au kutokuwa makini.
Pia lazima wakumbuke yule Mzungu Nooij
alituacha pabaya sana, angalau sasa tunaanza kuibuka, hivyo kazi dhidi ya
Nigeria haikuwa kila kitu, kazi ngumu zaidi ipo mbele yao, lazima waendelee
kujiandaa kwa kuwa mapambano ndiyo yameanza.
Nawashauri Taifa Stars wajue jukumu lao,
watambue imani ya Watanzania inavyoanza kurejea kwao na sasa ni wakati wa
kuhakikisha haturudi nyuma na badala yake tunasonga mbele tena na tena na wao
ndiyo madereva.
0 COMMENTS:
Post a Comment