LEO nianze kwa kushukuru, Watanzania wapenda
michezo ambao wamekuwa wakiniunga mkono kupitia maoni ambayo wananipa kupitia
mtandaoni.
Shukrani kwenu, najua wapo ambao tumekuwa tukitofautiana
kwa hoja, kwangu ni jambo jema. Wapo tunakuwa na mawazo sawa, jambo ambalo ni
zuri sana.
Kwa wale ambao wamekuwa wakisoma Mtandao wa
www.salehjembe.blogspot.com ninaoumiliki, pia shukurani kwa kuwa sasa unaongoza
kwa wasomaji.
Metodo ya leo inaangukia kwa wachezaji wa
kigeni ambao wanakuja nchini kwa ajili ya kucheza soka katika Ligi Kuu Tanzania
Bara ambayo ni ligi kubwa kuliko zote nchini.
Unakumbuka mwanzoni TFF wakati wa kipindi
cha Leodeger Tenga iliruhusu wachezaji 10, baada ya hapo ikakata idadi hiyo kwa
asilimia 50 na mwisho kuruhusu wachezaji watano tu huku ikisisitiza msimu
unaofuata, yaani msimu ujao, kutakuwa na wachezaji watatu tu wanaoruhusiwa kwa
kila klabu.
Idadi ya wachezaji 10 kukatwa hadi watano
ilizua mjadala mkubwa sana, wengi walipinga na mwisho ikazoeleka. Hofu kubwa
ikawa ni kwa wachezaji wa kigeni kupungua hadi watatu. Tenga aliondoka wakati
suala la wachezaji kushushwa tena hadi watatu likiwa limepita. Lakini TFF chini
ya Jamal Malinzi ikabadili upepo.
RAIS WA SIMBA, EVANS AVEVA AKIWA MAKAMU WAKE, GEOFREY NYANGE 'KABURU'. |
Ikafikia kwamba wachezaji waongezwe tena na
si kupunguzwa. Sasa kutoka watano hadi saba na hii ni baada ya klabu kuomba
waongezwe hadi kufikia kumi kama ilivyokuwa mwanzo. TFF ikaona angalau saba.
Wakati TFF inapitisha uamuzi wa kuwa na
wachezaji saba, Simba, Yanga, Azam FC na nyingine zinazosajili wageni
zikichekelea, kumeanza kuonekana rundo la vituko.
Yanga imemsajili beki Vincent Bossou kutoka
Togo, taarifa tunazo kashindwa kuonyesha kiwango katika mechi dhidi ya Mbeya
City. Taarifa zinazomtetea zinaeleza hakuwa na mazoezi muda mrefu, lakini
jiulize kweli mchezaji anayekwenda kufanya majaribio anakuwa hayuko tayari?
Kichekesho.
Simba wamemleta Papa Niang ambaye wakala
alikuwa akiwalazimisha wamsajili hata bila ya majaribio. Wamempa mechi moja tu
naye kituko, akacheza kama Bossou, dakika 45 tu nje, yuko hoi na taarifa
zinaeleza hakuwa fiti. Uozo mwingine huo, au kichekesho.
Yanga imemsajili Joseph Zutah, siku 10 tu
baada ya kumsajili, ikaamua kuvunja mkataba na raia huyo wa Ghana. Kwamba
haijaridhika na kiwango chake. Simba wakaleta Msenegali mwingine baada ya
Niang. Huyu jamaa anaitwa Abdoulaye Nd’aw, siku ya kwanza tu mazoezini, kala
mweleka, hoi. Eti hakuwa na mazoezi!
Hivi kweli Yanga na Simba wako ‘siriaz’
kweli. Vipi haya madudu ya kuleta wachezaji ambao hawako fiti, wanaokotwa tu,
hawana mazoezi na wanaingia mikataba ambayo inavunjwa ndani ya wiki. Au
wanaonyesha hawana lolote, hamuoni kuna tatizo?
Waungwana, hivi haya madudu yataisha lini
huoni Tenga alikuwa sahihi hadi kupunguza wachezaji wa kigeni wabaki watatu tu?
Vipi klabu zinalia na TFF kwamba ni tatizo!
Wachezaji wa kigeni wakija kucheza nchini ni
jambo zuri sana kwa maana ya changamoto na kujifunza, lakini kama watakuwa
wanaletwa wenye kiwango duni, wa kubahatisha basi hakuna hata hiyo maana ya rundo
la wachezaji wengi wa kigeni.
Huenda wangekuwa na nafasi chache wangeweza
kuwa makini wakijua nafasi ni chache mno. Iko haja Yanga na Simba kuonyesha
kupitia ukongwe wao kwamba wao ni makini zaidi katika masuala ya usajili.
Lakini iko haja ya kuonyesha Simba na Yanga
wanaweza kutambua gharama. Nilisikia wakisema wachezaji wanaokuja kufanya
majaribio wanakuja nchini kwa gharama zao.
Lakini hawawezi kutudanganya kwamba hawawagharamii
hata kidogo kwenye hoteli, chakula, usafiri wa ndani na kadhalika.
Itapendeza kama fedha wanazotoa ambazo
niseme zinapotea bure, basi wakawapa wazawa wanaofanya vizuri ili wainue morali
yao ya kiuchezaji kuliko kuendelea kuwabana na kupoteza kwa hao wageni wasio na
lolote.
Kingine, wakongwe muwe na kitengo maalum cha
kufanya utafiti wa uhakika wa wachezaji wanaokuja kabla ya kukurupuka na
kuwaleta hadi hapa nyumbani, halafu wanageuka kuwa kina Mr Bean!
0 COMMENTS:
Post a Comment