Ingekuwa siasa tungesema Simba, Yanga na
Azam zimeibuka na kuliandikia barua Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) kupinga agizo la kiasi cha dola 4,000 (Sh mil 8) kama malipo ya
kila mchezaji wa kigeni msimu huu.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi wiki kadhaa
zilizopita alitoa rai hilo kwa kila klabu yenye mchezaji wa kimataifa
kuhakikisha analipiwa kiasi hicho kwa ajili ya kuchangia mfuko wa maendeleo ya
soka la vijana, vinginevyo hawataruhusiwa kushiriki ligi kuu.
Kwa nyakati tofauti, viongozi wa Simba na
Yanga wamesema kuwa hawapo tayari kutoa kiasi hicho
kwani ni mpango wa TFF kutaka ‘kuwachuna’.
Katibu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha alisema
kwa pamoja (Simba na Azam) wameiandikia barua TFF kuomba kusitisha mpango huo
mpaka pale watakapotoa tamko.
Straika wa Yanga, Donald Ngoma, ni mmoja wa
wachezaji wa kigeni walioingia kwenye ligi kuu msimu huu na kukutana na kanuni
hiyo mpya.
“Sisi (Yanga), Simba na Azam tumewaandikia
barua TFF kuomba mpango huo usitishwe kwanza ili tuketi chini kulijadili, kisha
tutatoa tamko la pamoja kama klabu.
“Kwanza hakuna aliye tayari kuzilipa. Ni
kiasi kikubwa, lakini jingine ni mpango wa kutukamua tu hela. Badala ya wao
wawekeze kwetu (klabu), leo hii wanatutegemea sisi,” alihoji mhadhiri huyo wa
Chuo Kikuu Dar (UDSM).
Simba kupitia kwa kaimu katibu mkuu, Frisch
Collins, ilisema: “Kwa sasa hatuna jibu mpaka kamati itakapokaa, kisha
tutalitoa ufafanuzi.”
Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa
alipoulizwa kuhusu mpango huo, alisema Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za
Wachezaji, ndiyo itakuwa na jibu la mwisho wakati wa kupitisha majina ya
wachezaji wanaofaa kucheza ligi kuu msimu huu.
“Sina jibu la moja kwa moja, tusubiri kamati
hiyo ifanye kazi yake, mwisho wa yote ndiyo watatoa majina ya wachezaji
wanaostahili kucheza msimu ujao, kwa hiyo tusubiri jibu litapatikana tu,”
alisema Mwesigwa.
Mgawanyo wa fedha hizo ni kwamba dola 2,000
ni kwa ajili ya leseni ya mchezaji husika huku dola 2,000 nyingine ni kwa ajili
ya usajili (registration), kitu ambacho timu zimepinga vikali.
Kwa mpango huo inamaana Yanga, Simba na Azam
zenye jumla ya wageni 21, zitatakiwa kulipa zaidi ya Sh mil 160 huku timu za
Mbeya City, Stand na Coastal Union nazo zikikumbana na athari ya agizo la
Malinzi.
0 COMMENTS:
Post a Comment