Baada ya timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kutoka suluhu na Nigeria ‘Super
Eagles’, straika mahiri wa Simba, Mussa Hassan Mgosi, ameibuka na kusema kuwa
licha ya mabadiliko makubwa yaliyoonekana kwenye mchezo huo, matokeo hayo
hayajakata kiu ya Watanzania.
Mgosi amesema hayo kutokana na Watanzania wengi kuwa na kilio cha
muda mrefu kinachoilenga timu hiyo, ambapo wengi wangependa kuona timu hiyo
inakuwa katika ramani ya ushindani kama zilivyo timu kubwa za barani Afrika.
Ikumbukwe kuwa Stars na Super Eagles, zilivaana juzi Jumamosi
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, ukiwa ni mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki
Afcon 2017 nchini Gabon.
Mgosi alisema kuwa kwanza kabisa anampongeza kocha mkuu wa kikosi
hicho, Charles Boniface Mkwasa, ambaye ameonyesha kuwa anaweza kuifikisha mbali
timu hiyo kutokana na utofauti wa timu ambao unaonekana sasa, lakini akasema ni
lazima wachezaji wajiulize ni nini Watanzania wanahitaji, badala ya kufurahia
kutoka suluhu.
“Kama utakuwa muungwana hautapingana na mimi kwa hii kauli ya
kumsifu kocha wetu Mkwasa kwa mabadiliko aliyoyafanya kwenye kikosi cha Stars,
lakini ni wakati wa wachezaji sasa kujiuliza ni nini hasa Watanzania wanahitaji
kutoka kwao na siyo kutoka sare kwani hapo bado tuna kibarua kigumu kwa kuwa
wao watajipanga zaidi katika mchezo wa marudiano na hapo tutakuwa ugenini,
hivyo kujituma zaidi kunahitajika.
“Kiuhalisia mpira huwa haubadilishwi kwa siku moja tu, saa wala
dakika, bali ni mchakato ambao unahitaji uvumilivu lakini Stars inatakiwa kuwa
na uchu wa ushindi, hasa kwa kujituma kama wanavyofanya wengine,” alisema
Mgosi.
0 COMMENTS:
Post a Comment