October 23, 2015



MIMI ni Mtanzania kama wengine zaidi ya milioni 45 ambao tunaishi katika nchi yenye utajiri mkubwa kwa mambo mengi sana.


Nimezaliwa Tanzania, nimekulia Tanzania, bado ninaishi hapa Tanzania, ninaomba mwisho wa maisha yangu uishie hapa, nizikwe katika udongo wa taifa hili ninalolipenda moyoni.

Kama nimezaliwa, nimekulia, ninaishi pia ninatamani kuzikwa hapa Tanzania. Basi  ninaamini sina sehemu nyingine ninayoweza kuitetea, kuigombania kwa nguvu zangu zote zaidi ya nchi yangu.

Mimi ni Mtanzania ambaye nimekuwa nikijiuliza mengi kwa sasa. Kwamba kama uchaguzi wa keshokutwa usipokuwa salama, nitakimbilia wapi kwa kuwa sehemu ninaipenda kuliko zote kwa ajili ya kuishi ni hapa Tanzania.
Ndiyo maana nimekuwa nikipambana kueneza ujumbe wa amani kuhakikisha Tanzania inapita salama katika kipindi hiki kigumu bila ya kujali Watanzania wanamtaka huyu au yule, lakini kikubwa wachague kwa amani.

Timu yetu ya taifa, Taifa Stars ina kibarua kigumu kuwania kuchea Kombe la Dunia na Novemba 14 itakutana na Algeria jijini Dar es Salaam. Baada ya hapo, siku chache tu yaani Novemba 17, Stars itakuwa nchini Algeria kupambana na wenyeji.

Utaona ni mzigo mkubwa kwa Stars ambao hawajawahi kuupata huenda zaidi ya miaka 10 iliyopita. Nitakueleza kwa nini.

Kwanza Algeria, ndiyo timu bora barani Afrika kwa ubora wa viwango katika kipindi hiki. Algeria ni namba moja Afrika, inashika namba …..dunia. Tanzania ni namba …..Afrika, duniani ni namba……

Pili; Algeria ndiyo timu bora ya Afrika wakati wa michuano ya Kombe la Dunia 2014 iliyofanyika nchini Brazil.

Tatu; tunakutana na timu iliyoshiriki Kombe la Dunia zaidi ya mara moja. Unapozungumzia mbinu za kufuzu, watakuwa wanazijua. Ukizungumzia wafanye nini kwa wakati gani, wanajua zaidi ya sisi.

Nne; mechi zipo karibu sana. Tofauti ya siku tatu, kucheza na kusafiri, si kitu kidogo. Je, kwa wachezaji wetu wanaliweza hilo? Kuna mambo mengi sana ya kujiuliza.
Lazima tukubali kila Mtanzania atakuwa anataka kuiona Stars inafuzu. Lazima tukubaliane huu ndiyo wakati suala la utaifa linapaswa kuonekana zaidi kuliko wakati mwingine.

Mimi nimekuwa kati ya wale wanaokosoa sana katika suala la utekelezaji wa Taifa Stars. Safari hii nimejumuishwa katika kamati za kuisaidia Taifa Stars ishinde. Mimi ni mwenyekiti wa kamati ya uhamisishaji.

Lengo la kamati ni kuwahamasisha Watanzania kwa wingi kujitokeza uwanjani siku ya mechi. Naona hili linawezekana ndiyo maana nimetaka kuwakumbusha kwamba hakutakuwa na mafanikio kama tutatumia muda huu kulumbana sana.

Kamati hizi, hakuna maslahi, hazina hata bajeti ya fedha kwamba kuna watu wanafaidika. Hadi sasa karibu kila mjumbe anatumia muda na wakati mwingine fedha zake kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri.
Kuiunga mkono Stars ni jambo bora zaidi badala ya kufarakana. Siamini kama Algeria wamekuwa wakifanya vema wakiwa wametengana.

Tunaweza kuchagua wenyewe kwa kipindi hiki, kuonyesha uzalendo na Tanzania ifanye vema, jambo ambalo linawezekana. Au tukae na kuanza kupasua umoja ili tufeli.
Atajayefanya hivyo, hatakuwa Mtanzania mpenda nchi yake. Sitaki kuwafumba watu midomo, lakini unaweza pia kufumba mdomo kwa faida ya nchi yako katika kipindi ambacho suala la maslahi ya taifa linapewa kipaumbele.

Kimaisha, mambo yanabadilika, lakini suala la utaifa hata kwa mwenye uhakika wa kubadilisha utaifa wake, bado utaifa wa mwanzo hauwezi kuuondoa moyoni mwako.

Naipenda nchi yangu ndiyo maana niko tayari kusaidia. Wengine pia tuungane, tukishinda tuwe pamoja, tukishindwa tubaki pamoja. Hakuna linaloshindikana mnapokuwa pamoja.

Wako asiye mwoga

SALEH ALLY





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic