Katibu Mkuu wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mwesigwa Selestine leo amesaini
mkataba wa mwaka mmoja na mfuko wa huduma ya afya (NHIF) kwa ajili ya kutoa
huduma kwa wachezaji wa Ligi Kuu pamoja na viongozi wa benchi la ufundi.
Hafla ya kusaini
mkataba huo imefanyika katika hoteli ya Protea Courtyard iliyopo Upanga jijini
Dar es salaam ambapo katibu mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine na Mkurugenzi wa
Masoko na Utafiti wa NHIF Rehani Athumani walisaini kwa niaba ya pande hizo
mbili.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa uwekaji sahihi
mkataba huo, Mwesigwa amesema anaishukuru NHIF kwa kudhamini kutoa huduma ya
afya kwa wachezaji na mabenchi ya ufundi kwa vilabu vyote 16 vinavyoshiriki
Ligi kuu ya Vodacom.
Aidha, Mwesigwa
ameziomba klabu za Ligi Kuu Bara kutoa ushirikiano na watoa huduma ya afya
kwa wachezaji na viongozi kutoka NHIF pindi watakapokuwa wanafika kwenye vilabu
vyao kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Mkurugenzi wa Masoko
na Utafiti wa NHIF, Rehani Athumani akiongea kwa niaba ya mfuko huo
amesema wako tayari kufanya kazi na kutoa huduma ya afya kwa ngazi zote ikiwemo
kwa timu za madaraja ya chini pia.
TFF na NHIF
zimeingia mkataba wa mwaka mmoja wa udhamini wa huduma ya afya kwa wachezaji
kwa ligi kuu na viongozi wa benchi la ufundi, mkataba ambao unaeza kuongezwa
kila unapomalizika.
TFF kwa kupitia bodi
ya ligi inavitaka klabu zote za Ligi Kuu zitoe ushirikiano kwa wafanyakazi
wa NHIF katika kurahisiha shughuli za usajili ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa na
nyaraka sahihi zikiwemo picha za wahusika katika muda sahihi.
0 COMMENTS:
Post a Comment