Kufuatia tishio la Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika
(CAF) la kutaka kuifungia Zanzibar ushiriki wa shughuli za mpira duniani, Rais
wa TFF, Jamal Malinzi aliitisha kikao cha usuluhishi. Kikao hiki kilikuwa na
washiriki toka pande zote za mgogoro ambao ulipelekea mambo ya mpira kupelekwa
Mahakamani.
Kikao hiki kimefanyika leo katika Hoteli ya Courtyard Dar Es
Salaam chini ya Uenyekiti wa Rais wa TFF, Jamal Malinzi.
Baada ya kutambua
uzito wa suala lenyewe ambalo lingeweza kupelekea Zanzibar kukosa ushiriki
michuano ya CAF na CECAFA ili kunusuru soka la Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,
kikao kimefikia maamuzi yafuatayo:
1. Uitishwe
mkutano mkuu wa Zanzibar Football Association (ZFA) wa dharura kujadili
1.1 Mwenendo wa
kamati ya utendaji.
1.2. Mapato na
matumizi ya ZFA.
1.3. Kuteua kamati
ndogo ya kuandika upya Katiba ya ZFA.
2. Rais wa ZFA,
Ravia Idarus, kwa mujibu wa Katiba ya ZFA, ndiye atakeyeitisha mkutano huo.
3. Kamati ya sasa
inayoendesha ligi Zanzibar, itaongezewa wajumbe watatu watakoteuliwa na Rais wa
ZFA.
Ili maamuzi haya
yaweze kuwa na nguvu za kisheria na kikatiba, kikao kimeazimia kuwa mashauri
yote yaondolewe Mahakamani sasa na waliohusika kufungua mashtaka hayo
wamekubali kuyaondoa mara moja.
Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linazishukuru pande zote na wadau wote wa Mpira
wa Zanzibar waliowezesha kufikia hatua hii muhimu katika maendeleo ya Mpira wa
Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
0 COMMENTS:
Post a Comment