Baada ya Tumba Sued kutimkia Mbeya
City, Coastal Union sasa ipo katika harakati za kumbadili kiungo wake,
Abdulhalim Humud ili acheze beki ya kati iliyokuwa ikichezwa na Tumba.
Humud aliyewahi kutamba akiwa na
Ashanti United, Simba, Azam FC na Taifa Stars, anamudu kucheza nafasi ya kiungo
mkabaji na mshambuliaji kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya
Usajili ya Coastal Union, Salim Bawaziri, timu yake itasajili wachezaji wanne
tu katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo, lakini haitasajili beki.
“Tumba ameondoka na hakika hatutasajili
beki mwingine kuziba nafasi yake, badala yake tutamtumia Humud kucheza nafasi
hiyo akisaidiana na mabeki wengine Hamis Kibacha na Yusuph Chuma.
“Tunafahamu si kazi rahisi lakini ni
jukumu la mwalimu kuweza kulitimiza hilo na nafasi hii tumempa baada ya hivi
karibuni kurejea rasmi klabuni na kuungana na wenzake,” alisema Bawaziri.
Humud tangu aliposajiliwa amekuwa na
matatizo mbalimbali na kuna wakati alitoweka bila ruhusa na aliporejea alitakiwa
kuomba msamaha ndipo aliporejeshwa kikosini.
0 COMMENTS:
Post a Comment