HALL |
Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, amewachimba mkwara wachezaji
wa timu hiyo kuelekea mchezo dhidi ya Simba kwa kuwataka wasizungumze na na mtu
yeyote wa nje ya Azam FC kuhusiana na mechi hiyo ambayo presha yake imeshaanza
kupanda.
Simba na Azam FC zinatarajia kukutana wikiendi hii katika Uwanja
wa Taifa huku kukitarajiwa kuwa na upinzani mkali katika mechi hiyo ambayo kila
upande utahitaji kushinda ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya msimamo wa
ligi.
Msemaji wa Azam FC, Jaffar Idd, ameeleza kuwa kocha amewataka
wachezaji wote kutozungumza na mtu yeyote kuelekea mchezo huo na atakayebainika
amezungumza atakatwa mshahara.
“Kocha amewakataza wachezaji wote wa Azam kuzungumza kitu kuelekea
mchezo wetu dhidi ya Simba na hata mchezo mwingine wowote, jambo hili
limeandikwa hata kwenye mikataba yao, yeyote atakayekiuka agizo hili atakatwa
mshahara.
“Tumejiandaa vyema kuelekea mchezo huo na baada ya kurejea Tanga
tutaweka kambi ya pamoja na wachezaji tuliowaacha kwa ajili ya mazoezi ya
pamoja ya kuivaa Simba kwani lengo letu ni kuhakikisha tunashinda mchezo huo.
“Wachezaji wetu wote wa kimataifa wamesharejea tayari kwa ajili ya
mchezo huo akiwemo Wawa, Tchetche na Bolou,” alisema Idd.
0 COMMENTS:
Post a Comment