Kocha wa Azam FC, Stewart Hall amesema beki bora kwake ni Aggrey Morris na haoni jipya kwa Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani wa Yanga.
Hall ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumzia kuhusu beki bora wa kati raia wa Tanzania anayefanya vizuri katika timu za Ligi Kuu Bara.
Usisahau kuwa Hall amewafundisha mabeki wote wawili wakati akiwa Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes.
Hall alisema kuwa kuyumba kwa safu ya ulinzi ya timu yake inatokana na kumkosa beki wa wake, Aggrey Morris ambaye anasumbuliwa na majeraha ya goti.
“Morris ndiye beki bora kwa Watanzania wote wanaocheza ligi kuu, safu yangu ya ulinzi imekuwa ikifanya makosa mengi kutokana na kumkosa Morris ambaye ni majeruhi.
“Wawa anaonekana kufanya makosa mengi kwa kuwa Morris hayupo kwani ndiye aliyekuwa akimfutia makosa, niseme wazi kuwa Morris ndiye beki bora Tanzania hakuna mwingine,” alisema Hall raia wa Uingereza.
Morris aliumia katika mazoezi ya timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes iliyokuwa ikijiandaa na Kombe la Chalenji, mwaka jana. Hakwenda Ethiopia kushiriki michuano hiyo.
0 COMMENTS:
Post a Comment