February 20, 2016


Na Saleh Ally
UKITAKA kujua mechi ya leo kati ya Yanga dhidi ya Simba ni ngumu, basi soma makala haya yanayomhusu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe.

Hans Poppe anajulikana kwa kuwapa wakati mgumu Yanga kutokana na majigambo yake huku akisisitiza kwamba wana uhakika wa kuimaliza Yanga kila wanapokutana nayo.

Safari hii, Hans Poppe anasema mechi itakuwa ngumu na anaamini dakika 90 ndiyo mwamuzi wa mchezo huo wa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba ndiyo vinara wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 45 wakifuatiwa na Yanga wenye 43 huku Azam FC katika nafasi ya tatu ikiwa na 42.

Katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, Simba iliyokuwa mwenyeji ililala kwa mabao 2-0. Safari hii inahitaji kulipa kisasi, lakini Hans Poppe, anasema wako vizuri lakini Yanga nao anakubali wako sawa, hivyo haitakuwa mchekea kwa upande wowote. Ndiyo maana anasisitiza, mwamuzi ni dakika 90.


SALEHJEMBE: Vipi, mbona safari hii unaonekana kuwa na hofu?
Hans Poppe: Hapana, sina hofu hata kidogo. Ila najua Yanga hawakufika kileleni kibahati kabla ya sisi kuwang’oa.

SALEHJEMBE: Unafikiri kwa nini walifanikiwa kuwa kileleni?
Hans Poppe: Timu yao si mbaya, wana timu nzuri. Lakini kwa sasa Simba wako vizuri zaidi, ndiyo maana ninaomba washinde. Unajua walitufunga mzunguko wa kwanza, Waswahili wanasema: “Kwenda mjinga, kurudi je?”

SALEHJEMBE:Mwamuzi wa kati atakuwa ni mwanamama kutoka Kagera (Jonesia Rukyaa), unaona anaweza kulimudu pambano hilo?
Hans Poppe: Kweli sina uhakika, nilimuona kwenye Nani Mtani Jembe. Alikuwa na hofu sana, waamuzi wengi pia wamekuwa hivyo. Ningeshauri waamuzi waachane na hofu na kufanya kazi yao vizuri kwa kufuata haki.

SALEHJEMBE: Si waamuzi tu, ukifika wakati wa mechi hii, hata nyie viongozi pia mna hofu?
Hans Poppe: Kweli, hata viongozi na wachezaji pia. Vizuri kupunguza hofu na kila mmoja afanye mambo yake. Wakati mwingine mechi inapoteza radha kwa sababu ya hali hiyo ya hofu.


SALEHJEMBE: Lakini hauoni hofu inachangia kuongeza umakini wakati mwingine?
Hans Poppe: Hofu inachangia kuvuruga ubora wa mchezo. Utaona hata uchezaji unakuwa kama wa kubahatisha. Viongozi nao wanakuwa kwenye presha, mara wanawapokonya simu wachezaji, basi ili mradi tu.

SALEHJEMBE: Mwendo wa Simba kiasi unaridhisha, haukupi matumaini makubwa?
Hans Poppe: Yapo, katika mechi saba walizoshinda Simba, nimeona mechi sita. Timu inacheza vizuri tena mwanzo mwisho. Lakini naendelea kusisitiza mchezo utakuwa mgumu, ni vizuri vijana wajitume na Wanasimba wawaunge mkono.

SALEHJEMBE:Simba inacheza vizuri, lakini fowadi ya Yanga, hasa Donald Ngoma na Amissi Tambwe ni hatari kwa afya ya ulinzi wa Simba, unaliona hilo?
Hans Poppe: Kweli, ni wazoefu na wazuri. Tambwe yuko vizuri, Ngoma pia ni mzuri ila pia akitulia, la sivyo hawezi kucheza.

SALEHJEMBE: Kivipi hawezi kucheza?
Hans Poppe: Ngoma ni mchezaji mwenye nguvu na kasi, msumbufu kwa mabeki. Lakini si mstahamilivu, akiwa na presha tu, basi hawezi kucheza.
Championi: Lakini mna walinzi bora?
Hans Poppe: Ndiyo, tunao ndiyo maana uliona mechi iliyopita alilazimika kumpiga Hassan Kessy.


SALEHJEMBE:Lakini suala hilo lipo TFF tayari, hupaswi kuwa na hofu nalo…
Hans Poppe: Ndiyo, lakini tangu mzunguko wa kwanza. Hakika mimi sina imani na TFF, mara nyingi nasema ipo kwa ajili ya kuibeba Yanga na wengi hawaamini hilo lakini ndiyo hali halisi.

SALEHJEMBE: Vipi kuhusiana na suala la kuwapa motisha wachezaji wenu, mechi hii ina mshawasha wa aina yake.
Hans Poppe: Hilo litafanyika, viongozi tunajua tulifanye vipi. Lina wakati, litafanyiwa kazi.

SALEHJEMBE: Halafu nasikia upo Lubumbashi (DR Congo) kufuatilia fedha za mgawo wa mauzo ya Mbwana Samatta?
Hans Poppe: Ahaaa…. eheee! Hapana ila nipo huku (Lubumbashi) kufuatilia mambo yangu, hilo la Samatta linashughulikiwa vizuri na uongozi.

SALEHJEMBE: Niwatakie mechi njema.

Hans Poppe: Ninashukuru.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic