Na Saleh Ally
IDADI kubwa ya wadau wa soka hapa nyumbani Tanzania, England na kwingineko duniani wanajiuliza swali moja tu muhimu. Kweli Manchester United itakubali kuwa ngazi, ipigwe na Leicester City iwe bingwa wa England kwa mara ya kwanza?
Kama Leicester ambayo iko ugenini kesho kwenye Uwanja wa Old Trafford itashinda dhidi ya Man United, basi itakuwa imefikisha pointi 79 tofauti ya pointi 10 dhidi ya Tottenham Hotspur ambao wanashika nafasi ya pili.
Kama ni hesabu, inaonekana hivi, ni lazima Leicester watakuwa mabingwa wa England msimu huu. Kama ni miujiza, basi ina uwezo wa kuwazuia kwa asilimia 10 pekee, kwa kuwa mpira nao hauaminiki.
Lakini kusema lazima watakuwa mabingwa, bado inawezekana kwa asilimia 90. Kwani hata kama kesho watapata sare dhidi ya Man United, bado wanaweza kutangazwa mabingwa rasmi keshokutwa Jumatatu kama Tottenham watapoteza mchezo wao dhidi ya Chelsea wakiwa ugenini Stamford Bridge.
Hata hivyo, bado mechi ya kesho ndiyo inabaki kuwa kila kitu kwa Leicester ambao kama watabeba ubingwa, basi ni wachezaji hadi kocha watakuwa wameweka rekodi na kufanya mabadiliko huku wakiweka kumbukumbu ya Blackburn Rovers iliyopanda daraja na kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 1994-95.
Mechi zilizopita:
Manchester United haina nguvu ya kufukuzana na Leicester kama utazungumzia ubingwa lakini katika mechi zake sita zilizopita, imeshinda nne na kupoteza mbili. Leicester imeshinda tano na sare moja.
Kwa mwendo, Leicester wako vizuri zaidi lakini kamwe hauwezi kuwabeza Man United kwa kuwa mwishoni kikosi chao kinaonekana kuwa vizuri zaidi na wamefanikiwa kuingia fainali ya Kombe la FA.
Ugenini:
Leicester ni kati ya timu bora zinapokuwa zinacheza ugenini. Kwani kati ya michezo 12, imeshinda mechi 10, imetoka sare 1 na kupoteza 1. Hii inaipa asilimia 71 za ushindi inapokuwa nje ya nyumbani.
Hivyo katika pointi zake 67 katika msimamo sasa, 31 imefanikiwa kukusanya ikiwa ugenini. Hili si jambo dogo na Man United hawapaswi kuibeza Leicester hiyo kesho.
Kwa Manchester United, wakiwa nyumbani inaonekana hivi; katika mechi 11, wameshinda 11 bila sare au kupoteza. Maana yake wana asilimia kubwa zaidi ya kufanya vizuri nyumbani.
Mechi hii itakuwa burudani ya aina yake na huenda ikawa gumzo kwa kuingia kwenye historia ya soka la England.
Presha:
Katika mechi hiyo, wanachotaka Manchester United ni kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, yaani Top Four, japokuwa bado watakuwa hawataki kugeuzwa ngazi hiyo kesho na kuingia kwenye historia kuwa wa mwisho ‘kuisaidia’ Leicester kuwa bingwa.
Kwa Leiceter, lazima watakuwa kwenye presha kubwa kidogo ambayo inaweza kuwa msaada au tatizo kwao. Kuwa mabingwa ni jambo ambalo wana hamu kubwa, pia wana hofu kuu ya kufungwa. Haya wakiyachanganya vibaya, huenda yatawaangusha na wakashindwa kucheza mpira wao.
Mechi 5:
Katika mechi tano za mwisho ambazo Man United imecheza. Imefanikiwa kufunga mabao manne ikafungwa matatu wakati ilipopoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Tottenham. Man United inaonekana iko makini kwenye ulinzi, lakini ikiotewa, kweli inalainika.
Leicester, mechi zao tano wamezicheza hivi, wameshinda mabao tisa, wakaruhusu mabao manne. Aina ya uchezaji inaonekana ni ‘open game’. Mchezo ambao si wa ulinzi mwingi sana na wanaweza kukufunga mabao mengi ukizubaa lakini wanafungika.
Mara ya mwisho:
Mara ya mwisho zilikutana Novemba 28, mwaka jana ikiwa ni mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu England. Matokeo yalikuwa 1-1 licha ya Man United iliyokuwa ugenini kwa bao la kusawazisha la kiungo Mjerumani Bastian Schweinsteiger.
Hii inaonyesha hata mechi ya kesho, haitakuwa rahisi kwa kila timu. Ingawa Leicester lazima wacheze wakitaka ushindi hata kama sare inaweza kuwapa ubingwa.
Wanakosekana:
Kila upande utakosa watu muhimu, wageni Leicester kama kawaida, mshambuliaji wao nyota Jamie Vardy anaendelea kutumikia adhabu ya kufungiwa. Walimkosa katika mechi iliyopita dhidi ya Swansea, lakini wakashinda 4-0 wakiongozwa na Riyad Mahrez.
Manchester nao wana kazi kidogo, wanaendelea kuwakosa wachezaji kama Schweinsteiger aliyewakomboa wakiwa ugenini dhidi ya Leicester. Pia Luke Shaw, Will Keane na Adnan Januzaj nao wanakosekana. Hawawezi kuwa athari kubwa kwa Man United kwa kuwa wamekuwa nje kwa mechi kadhaa na imeendelea kupambana.
Wabetishaji:
Kampuni nyingi za kubeti za England zinaonekana kutoa nafasi kubwa kwa Man United kushinda mechi hiyo, wakiamini presha kubwa itawamaliza Leicester.
Inaonekana wanaocheza mchezo huo, wengi wamechanganyikiwa, lakini wahusika wakuu, wamewapa nafasi Man United kwamba wana nafasi kubwa kutokana na mwendo.
Ingawa wafanyabiashara wa ubetishaji, pia ni wajanja wanaweza kulalia wanakoona, kutaharibika ili kutengeneza biashara yao.
0 COMMENTS:
Post a Comment