April 8, 2016Na Saleh Ally
SAUTI za viongozi wawili wa juu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zimesikika wakijadili namna ambavyo wanaweza kuisaidia timu moja kupata ushindi.
Viongozi hao, wanaeleza wanavyotaka kitita cha fedha, Sh milioni 10, walipwe viongozi wengine, Sh milioni 10, nyingine kwa ajili ya moja ya kamati za TFF na baada ya hapo Sh milioni 5, ambayo atapewa ofisa mwingine wa shirikisho hilo ili aende kuzungumza na wakubwa wa Idara ya Uhamiaji ambako inatakiwa kumkandamiza mchezaji wa timu fulani ili nyingine ipate ushindi.

Siku moja tu baada ya sauti hizo kusikika, Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Martin Chacha akatangaza kuachia ngazi, huku akisema ni kutokana na kubanwa na matatizo ya kifamilia.

Gazeti hili likafanya mahojiano na Juma Matandika, kutaka kujua vipi alishiriki kwenye kikao hicho, akasisitiza anaamini sauti zao zimeigizwa kwa kuwa na watu wengi wana uwezo wa kuigiza huku akimtaka mwandishi kama naye anataka sauti yake iigizwe, basi aende ili ampeleke.Tuliacha hilo, tuamini kabisa Rais wa TFF, Jamal Malinzi, hawezi kuhusika na kitu kama hiki na waliokwenda kutenda jambo hilo walifanya bila ya kumueleza kwamba wana ujanja wanaofanya. Lakini najiuliza, yeye atalikwepa vipi?

Wote tunajua suala hili linahusiana na rushwa, adui wa haki, adui wa mpira wa Tanzania na adui wa nchi yetu, lakini naona kuna ujanja unafanyika kuona hili linaonekana limetengenezwa.

Najua lazima Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) haitaliacha lipite hivihivi na hasa ukizingatia serikali ya sasa ni ile inayotaka mambo yaende kwa haki na uamuzi wake ni haraka, si kama ilivyokuwa katika awamu nyingine zilizopita za uongozi.

Nimeanza kuona harufu ya njama zinazoanza kutengenezwa kutaka kulifanya jambo hili lionekane ni bahati mbaya au halikuwahi kabisa kutokea.


Kuna mipango inatengenezwa ili ionekane kwamba waliosikika sauti zao zimetengenezwa na kuna lengo la kuwadhalilisha. Lakini naona hata TFF yenyewe inataka kuingia mkenge kutaka kuanza kuzuia vyombo vya habari kuliripoti jambo hili, niwahakikishie mtafeli.

Huenda ni njia ya kutaka kutulazimisha kwa ulaini kuamini maelezo ya Matandika? Kwamba sauti zao zimetengenezwa? Jamani, uoneeni huruma mpira wa Tanzania nanyi muwe na aibu kiungwana!

Niliona taarifa yao waliyoitoa TFF siku moja baada ya sakata hilo, wakisisitiza kwamba wanaonya viongozi wa juu wa shirikisho hilo kuhusishwa na sakata hilo.

Kwangu ninaona ni kuingilia uhuru wa vyombo vya habari, kwangu naona ni kulazimisha kuwafumba midomo waandishi wa habari kwa lengo la kufunika maovu kwa nguvu, jambo ambalo haliwezi kuvumilika wala halitakuwa na nafasi kwangu.

Sauti zinazosikika, zinajulikana ni za kina nani. Wanaozungumza ndiyo viongozi wa ngazi za juu. Sasa unashindwa vipi kuwahusisha na viongozi wa ngazi za juu?

Viongozi wa ngazi za juu wanakwenda vipi katika hili na wengineo wametajwa ndani yake. Hata kama waliotaja ingekuwa hatuwajui, basi isingekuwa rahisi kuruka maneno waliyosema hasa yale waliotaja viongozi wa juu wa TFF.

Ninachomshauri Rais wa TFF, Jamal Malinzi ni kujiandaa. Kuwa tayari, kukaa mguu sawa kama itathibitika wahusika walichofanya kupitia vyombo vya dola, basi yeye ajivue madaraka kwa kuwa atakuwa amechafuliwa na aliowaamini.

Tulilalama kuhusu tuhuma za rushwa kwenye soka, sasa tuhuma ziko ndani ya shirikisho, waliopewa dhamana ya kuuendesha mpira, nini maana yao wao kuwepo? Kwani waliojiuzulu wote ni wale waliopatikana na hatia tu, kuhofiwa ni kuondolewa kwenye uadilifu tena kwa njia kama hiyo ya sauti.

 Hii ndiyo kashfa kubwa zaidi kutokea katika shirikisho hilo tokea kuanzishwa kwake. Nakumbuka kiongozi wa Chama cha Soka Tanzania (Fat), alifungwa jela.  Lakini TFF haikuwa imewahi kuchafuka kwa kiwango hiki.

Tena inachafuka kipindi ikiwa imetoka kutoa adhabu kupitia moja ya kamati zake ambayo iliwafungia wachezaji, waamuzi na viongozi kwa madai ya kupanga matokeo. Haki iko wapi sasa?


Badala ya kupambana kuizima, kwa kutaka kuwaziba watu midomo kwa nguvu. Huu ni wakati wenu wa kutafakari na kutengeneza mwisho wa kuongoza kwa matamanio ya maendeleo ya nafsi zenu na kuwaacha wenye nafasi ya kuongoza kwa lengo la kuleta maendeleo kwenye mpira wa Tanzania. Leo nimeanza, kesho nitarudi tena, nina mengi ya kusema.

2 COMMENTS:

  1. Kwanza jiuzuru wewe Saleh kutoka Global kabla ya Malinzi kuchukua uamuzi mgumu

    ReplyDelete
  2. Ndi matatizo ya kuongoza soka kwa kujuana,matokeo yake watu wanafanya kazi kwa mazoea.TFF imekuwa na tabia ya kuajiri watendaji waliofukuzwa Yanga,Simba na Azam matokeo yake hakuna tofauti ya TFF na vilabu kama ilivyokuwa Enzi za Tenga.Leo hii kocha wa timu ya Taifa hajalipwa mshahara wa miezi tisa halafu Rais wa Shirikisho anasimama hadharani bila aibu anasema kocha wa timu ya Taifa ni sawa na waajiriwa wengine wa TFF ambao hawajalipwa mshahara.Halafu tunatarajia kocha huyo huyo aipeleke Taifa stars fainali za Afcon 2017?Leo hii madeni kila kona ikiwemo TRA.Uongozi unaoshindwa hata kupanga ratiba ya ligi kuu unastahili kuendelea kuwepo madarakani?Hivi inakuwaje marefa wafungiwe kwa kupanga matokeo halafu aliyewapanga kuchezesha mechi hizo asiguswe?Naomba wadau wa soka wamuombe mzee Tenga madarakani ili aje arudishie heshima ya Shirikisho hili kwa miaka miwili iliyobakia

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV