June 25, 2016


Yanga itakuwa dimbani Jumanne ijayo kuwavaa TP Mazembe katika mechi ya Kundi A ya Kombe la Shirikisho Afrika linaloandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) dhidi ya TP Mazembe, hofu kubwa ya timu hiyo ni beki ya kushoto.

Wachezaji wawili wanaocheza nafasi hiyo, Haji Mwinyi na Oscar Joshua wote wapo katika hatari ya kuikosa mechi hiyo, hivyo Yanga ipo katika wakati mgumu wa nani acheze nafasi hiyo.

Mwinyi yeye ana kadi nyekundu aliyoonyeshwa katika mchezo uliopita wa michuano hiyo dhidi ya MO Bejaia ya Algeria wakati Joshua ana maumivu ya nyama za paja, pia aliyapata katika mchezo huo.

Habari njema kwa Yanga ni kwamba, Joshua tayari ameanza mazoezi mepesi kambini huko mjini Antalya, Uturuki ambako timu hiyo imejichimbia kujiandaa na mechi dhidi ya TP Mazembe.

Kutoka Uturuki, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alisema: “Joshua anaendelea vizuri na tayari ameanza mazoezi mepesi kwa ajili ya kujiandaa na mechi na Mazembe.

“Bado sijajua hatma yake kama atacheza au hatocheza mechi na Mazembe, hivyo kila kitu kitajulikana ikiwa imebaki siku moja kabla ya mchezo wao baada ya daktari wetu Edward Bavo kutoa ripoti yake.”

Joshua alipata majeraha hayo usiku wa Jumapili iliyopita dakika ya 32 katika mchezo dhidi ya MO Bejaia mjini Bejaia, Algeria ambapo ilibidi atolewe na nafasi yake kuchukuliwa na Mwinyi. Katika mchezo huo, Yanga ilifungwa bao 1-0.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV