July 13, 2016


Kiungo Mganda aliyetemwa na Simba, Mganda, Brian Majwega, amejiunga na KCCA ya Uganda na kupewa mkataba wa miaka miwili.

Majwega ambaye ameachwa na Simba baada ya msimu wa ligi uliomalizika Mei, mwaka huu, ameamua kurudi KCCA ambayo alijiunga nayo mwaka 2009 kabla hajachukuliwa na Azam, Januari, 2015.

Kutokana na kutokuwa na msimu mzuri tangu atue Azam, klabu hiyo ikamrudisha kwa mkopo KCCA kabla ya kuzinguana na Azam na kuibukia Simba, Januari, mwaka huu na kucheza kwa takribani miezi sita kabla na baadaye kuachwa.

Akizungumzia urejeo wake ndani ya KCCA, Majwega alisema: "Najisikia furaha kurudi nyumbani na nimepokelewa vizuri. Kwa kushirikiana na wachezaji niliowakuta hapa naamini nitazidi kupata mafanikio makubwa zaidi.

"Nilipokuwa Tanzania kwenye timu za Azam na Simba kulinifanya kujifunza mengi ikiwemo jinsi ya kufanya kazi na makocha na wachezaji kutoka mataifa mbalimbali, naamini nafasi hiyo itaniongezea kitu ndani ya KCCA kuelekea kuchukua mataji.”

Mtendaji Mkuu wa KCCA, David Tamale amesema kitendo cha wao kumrejesha Majwega klabuni hapo ni ishara kwamba wanavutiwa na kazi yake huku wakiamini ataongeza chachu ya mafanikio kwao.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV