July 13, 2016Zaidi ya asilimia 90, Azam FC inataka kuachana na fowadi wao, Kipre Tchetche, kutokana na utovu wa nidhamu aliouonyesha kwa kutojumuika kambini mpaka sasa, ikiwa ni wiki moja.

Taarifa za chinichini zinadai chanzo cha yote, fowadi huyo raia wa Ivory Coast analazimisha kutaka kuondoka kikosini hapo na kwamba amekuwa akirubuniwa na timu za ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Yanga ndiyo imehusishwa zaidi na kumshawishi mchezaji huyo bora msimu 2013/14, wakitaka achukue nafasi ya Donald Ngoma ambaye amezidi kuitoa udenda Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini.

Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba amekiri Kipre kutofika kambini mpaka sasa na kwamba katika mawasiliano yao hajatoa sababu za msingi za kuchelewa, hali inayowapa wasiwasi analazimisha kuondoka.

Kawemba ameweka bayana kuwa iwapo kweli kuna timu inamrubuni, basi ijitokeze kununua lakini akasisitiza thamani yake ni dola 150,000 (Sh milioni 322.1).

"Hajafika mpaka sasa na kila tukiwasiliana naye anatuambia anakuja leo, kesho na hafiki. Sasa hatujui anawaza nini lakini ifahamike bado ana mkataba na Azam wa mwaka mmoja na kila kitu juu ya mikataba yake tunacho sisi.

"Kama kweli anataka kuondoka, thamani yake ipo wazi. Dola 150,000 na bahati nzuri wachezaji wetu wote kila mmoja thamani yake ipo kwenye mkataba anaousaini.

"Iwapo kuna timu inamtaka, ije inajua kabisa thamani yake ni ileile iliyo kwenye mkataba wake," alisema Kawemba na kusema kuwa Yanga hawajajitokeza hadharani.


Licha ya hivyo, Kawemba akasisitiza kuondoka ama kutoondoka kwake hilo wanaliacha mikononi mwa Kocha Zeben Hernandez.

SOURCE: CHAMPIONI

1 COMMENTS:

  1. Nyie si mlituonyesha picha Kipre akisaini umangani,sasa iweje tena muigeukie Yanga?Au Yanga wamekuwa waarabu wa Dar!?

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV