July 13, 2016


Na Saleh Ally
GUMZO kubwa kwa takribani wiki moja iliyopita ni kuhusiana na mzozo kati ya Yanga na Shirikisho la Soka Tanzania maarufu kama TFF.

Mwishoni mwa wiki hiyo ya mzozo, ulihamia kwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Yanga, Jerry Muro na mwisho akafungiwa kufanya shughuli za soka kwa mwaka mzima.

Ukifuatilia kwenye maoni ya watu wengi kuna msigano wa mawazo, wengine wakiamini Muro acha afungiwe, wengine wakipinga kabisa, kwamba TFF sasa imepitiliza ubabe.
Kamati ya Maadili ya TFF ambayo mwenyekiti, makamu wake na wajumbe waliteuliwa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi ndiyo walioamua adhabu hiyo ya Muro bila ya yeye kujitetea.

Walimwita awali, akafika pale na kueleza mapungufu ndani ya barua ya wito ambayo iliandikwa ilimradi na Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine. Ikaonekana kweli ni barua ya hovyo, ikaandikwa nyingine kipindi cha sikukuu, Muro hakuwepo na mwisho alitoa maelezo kwamba alikuwa kwao mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya sikukuu.

TFF inamfungia Muro mwaka mmoja ikiwa ni baada ya mwaka mmoja kumfungia Dk Damas Ndumbaro kwa ujanjaujanja wa namna hiyo, maana aliitwa wakati akiwa safarini Ujerumani, akafungiwa bila ya kujitetea!

Dk Ndumbaro alifungiwa wakati akizitetea klabu zipate haki yao. Hakuna klabu iliyompigania baadaye, lakini ukweli alionekana ni ‘tatizo’ kwa uongozi wa TFF kwa kuwa alianza kusikilizwa sana, alionekana mtenda haki na inawezekana hoja zake zilianza kuuelemea upande wa pili ambao unajua mambo yake mengi si sahihi.

TFF inajijua kwamba kiutendaji sasa ni dhaifu, inajua imeandamwa na kashfa kibao ikiwemo ile ya suala la upangaji matokeo, tuhuma ambayo inaonekana kuzungushwa bila ya majibu bila sababu za msingi. Hakuna anayeifungia TFF kwa madudu kibao na inaendelea kufanya mengine.

Tokea amefungiwa Muro, siku nne zilizopita hadi jana mchana hata ile hukumu haikuwa imetoka kwa maandishi na hii ilitokana na Muro kuonekana mjanja, mwelewa na anajua wapi wameboronga.

Kumekuwa na taarifa kwamba inarekebishwa ili kuendana na hoja za Muro ambazo aliziibua mara tu baada ya kufungiwa. Lakini usisahau, TFF imemfungia Muro bila ya kumhoji lakini kitu kibaya zaidi, hoja zilizoonekana kwao ni ‘matusi’ hawakuwahi kuzijibu.

Pamoja na mengi, lakini yale ya Muro kusema hawawezi kuilipa TFF kwa kuwa hawakuingiza kipato, wala hawana sababu ya kulipa kodi kwa kuwa hakuna kilichoingia imeonekana ni kashfa lakini TFF ilishindwa kujua hilo, ikapeleka barua ndefu yenye uchanganuzi ikitaka nayo ilipwe.

Hii ishu ilikuwa ni ule uamuzi wa Yanga kuamua mashabiki wake waingie bure katika mechi dhidi ya TP Mazembe. Kitu kibaya zaidi, TFF ilionekana kutojua mengi yakiwemo ya kutaka Mamlaka ya Mapato (TRA) nayo ilipwe, lakini yenyewe ikatoa tamko kwamba hakuna wanachotakiwa kulipwa kutoka Yanga.

Kingine cha kushangaza kinachoonekana TFF ni yenye visasi ni hiki; imemfungia Muro haraka sana wakati inaonyesha wazi ina hasira na imechukizwa na kutopata kitu cha mgawo kwa kuwa mashabiki waliingia bure.

Dk Ndumbaro alifungiwa katika hali hiyohiyo na kinachoshangaza zaidi ni kuona mashabiki wanalichukulia suala hilo kishabiki! Kwa kifupi, kama unamuona Muro hana akili lakini TFF haitaki kuona wanaoizidi akili au hoja. Na huwezi kupinga kwamba wahusika hasa kamati, nao hawatendi haki huenda pia kuna haja ya kuangalia au kubadili katiba, wanakamati wasiteuliwe na Rais wa TFF ili kuepuka ‘kutekeleza jambo la bwana’.

Nilihoji hivi; kesi ya Donald Ngoma kumpiga kiwiko Hassan Kessy akiwa Simba, hadi leo haikuwahi hata kufanyiwa kazi. Lakini kwa kuwa Muro aliikosoa TFF na kuitoa jasho huku akionekana anawazidi maarifa kwa hoja, wamemfungia kwa kutafuta ‘vikosa’ ilimradi ili kutimiza lengo.

Mnaoshangilia leo, mnaipa TFF nguvu ya kumfungia kila inayeona amekuwa kigezo au kigingi kwao kwa kuwa mambo yao mengi yanaonekana hayana ‘akili’ sahihi iliyolenga kuleta maendeleo.

 Nani anaweza kusimama hadharani akainua mkono na kusema TFF chini ya Jamal Malinzi, imeleta mabadiliko ukilinganisha na ile la Leodegar Tenga?
Lakini ukiuliza wangapi wanaona TFF ya Malinzi imeturudisha nyuma na afadhali ile ya Tenga, rundo la mashabiki wapenda soka watajitokeza kuinua vidole na kusema ni kweli.

Itakuwa jambo jema kuangalia hoja za msingi katika ufungiwaji wa Muro. Sina haja ya kumtetea, tena naona kama hukumu hiyo inatumia vigezo vya zamani. Wote tunajua Muro naye amekuwa akiboronga mara kibao kwa kuzungumza kwa jazba au maneno ya mbwembwe bila hata sababu ya kufanya hivyo.


Achana na hayo ya awali, maana hawakuwahi kumshitaki. Katika hili la bure, kipi hasa kilikuwa kibaya? Kusema watu watakaa juu ya paa, ndiyo kosa la kumfungia mtu mwaka mzima? Kumbukeni, mzigo wa Muro wa Yanga, kesho utahamia kwa nanihii wa Simba, Mtibwa Sugar au Stand United. Maigizo matupu!

3 COMMENTS:

  1. HALI NI MBAYA TFF,HAKUNA ASIYEONA,BASI KWA NINI WAZIRI MWENYE DHAMANA NAE YUKO KIMYWA?

    ReplyDelete
  2. NI KWELI TFF IN MAPUNGUFU MAKUBWA LAKINI HOJA YA KUWA "Muro hakuwepo na mwisho alitoa maelezo kwamba alikuwa kwao mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya sikukuu." HAINA MASHIKO, UNAPOSEMA HAKUWEPO UNAMAANISHA ILITAKIWA APEWE BARUA AKIWA WAPI? JE UMEWAHI KUJIULUIZA NI KWANINI Dk. NDUMBARO KAAMUA KUPIGA KIMYA! NAPENDA KUKUHAKIKISHIA KUWA KISHERIA JERRY MURO ALIPOKEA WITO WA KUITWA KWENYE KAMATI ILI ASIKILIZWE LAKINI HAKWENDA.

    ReplyDelete
  3. Ngoja tuone hii movie,ila ukweli TFF wameingia choo kisichowahusu.

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV