July 15, 2016Simba ipo kambini mkoani Morogoro ikijiandaa na msimu ujao wa 2016/17, lakini habari nzuri ni kuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog anaonekana kuwa ‘serious’ na kazi yake, ndiyo maana akaamua kikosi chake kikajifiche nje ya mji mkoani hapa.

Championi Ijumaa ambalo ni gazeti pekee kufika kwenye kambi hiyo iliyopo eneo la Highlands ambapo kuna taasisi ya dini, imeshuhudia mchakato unavyoendelea ambapo sura za wachezaji wa timu hiyo zinaonekana kuwa katika hali ya furaha na kufurahia kile ambacho wanaelekezwa na benchi lao la ufundi.

Katika mazoezi ya jana asubuhi, Simba ambayo imekuwa haifanyi vizuri kwa misimu minne mfululizo, wachezaji wake hawakuwa na kazi kubwa ya kufanya, Omog alionekana akitoa maelekezo zaidi kuliko wachezaji kucheza mpira huku utulivu wa mazingira ukionekana kuwa wa kiwango cha juu kama vile timu ipo Ulaya ambapo kunasifika kuwa na sehemu nzuri tulivu na zenye viwanja bora vya mazoezi.

Saa 2:30 asubuhi ratiba ilianza kwa wachezaji wa Simba kufika uwanjani wakitokea kwenye vyumba ambavyo vipo eneo hilohilo, walifika na kuanza mazoezi ya viungo.

Baadaye wakaanza kuruka koni, walipomaliza hapo wakaanza kuuchezea mpira kidogo, kisha wakawa wanapiga mpira kwa vichwa katika staili ya kuonyesha uwezo wao wa kumiliki mpira.

Baada ya hapo wakarushiana mpira kwa muda kidogo, kisha wakakusanyika katikati wakaanza kunyoosha viungo na kuanza kupewa maelekezo muhimu na Omog.

Omog alichukua muda mrefu kudogo kutoa maelezo huku akishirikiana na msaidizi wake, Jackson Mayanja raia wa Uganda. baada ya hapo wakaondoka na kurejea kambini.

Mazingira ya kambi hiyo ni mazuri, nyasi za uwanja wanaofanyia mazoezi ni nzuri na zenye kiwango bora, pia kuna hali ya utulivu na kila mmoja ambaye anakuwepo mazoezini anaonekana kufanya majukumu yake bila kufokewa wala kupigiana kelele akiwemo daktari wa timu hiyo, Yasini Gembe. 


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV