July 15, 2016



Na Saleh Ally
TAYARI Kocha wa Simba, Joseph Omog ameamua kikosi chake kifanye mazoezi kimyakimya. Hataki mashabiki wala waandishi wa habari.

Omog amesema hataki wachezaji wake wawe na presha, kwa kuwa kutakuwa na mashabiki wengi ambao watawafanya wacheze kwa kuwaridhisha wao.

Huenda ni wazo zuri sana, ingawa sijui kipi kinamfanya akataze hata waandishi kuingia angalau kuangalia kazi yake kwa dakika 10 pekee. Huenda kwa kuwa hajiamini kwa kuanzia, anaweza kupewa muda.

Suala la mazoezi linaweza lisiwe ishu sana, lakini mambo yatabadilika Simba itakapoanza kucheza mechi za kirafiki na baadaye mashindano.
Ligi Kuu Bara itaanza wiki ya pili ya Agosti, maana yake ni mwezi mmoja pekee umebaki hadi kufikia siku yenyewe. 

Hauwezi ukawa muda mwingi sana kwa Omog na kikosi chake na lazima wafanye kazi kwa juhudi na maarifa kwa kuwa wanakitumikia kikosi chenye madeni mengi na makubwa.

Wanachama wa Simba wanaidai klabu yao ubingwa, msimu wanne wa Ligi Kuu Bara. Usisahau pia misimu hiyo yote, Simba haijashiriki michuano ya kimataifa hasa ile iliyo chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Kama hiyo haitoshi, mashabiki wa Simba ambao wanaonekana kuwa wavumilivu zaidi wangependa kuiona klabu yao inashinda na kurejesha furaha yao.

Hakuna ubishi Omog lazima ajue klabu anayoifundisha ni tofauti kabisa na Azam FC kwa mambo mengi sana na hasa suala la utamaduni. Presha ya mashabiki na wale wanaotaka kuona timu yao inashinda tu. Ndiyo maana nimesema wale wa Simba ni wavumilivu sana.

Kuna deni la ziada, Kombe la Shirikisho. Kuanzia msimu uliopita limeanzishwa na mshindi, anapata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho barani Afrika. Nalo Simba wangependa kuona wanafanikiwa kulipata maana limeanza, watani wao Yanga wamelichukua.

Historia inaonyesha mara nyingi Simba imekuwa ikichukua makombe ya karibu kila michuano mikubwa inapoanzishwa. Safari hii wakati Kombe la Shirikisho linaanza, wamekuwa vibaya na wale wa ‘kuonewa’ tu.

Uongozi wa Simba umeonekana kujitahidi kila namna, kwa usajili unavyoonekana hauwezi kusema mbaya kwa kuwa karibu kila sehemu iliyoonekana ina tatizo wameifanyia kazi.

Vizuri zaidi, wametoa nafasi kwa kocha mpya ambaye ni Omog kuwaangalia wachezaji wa nyumbani na wale wa kigeni, pia awe na nafasi ya kusema huyu hapana au ndiyo na ana nafasi ya kuongeza mchezaji kwa mapendekezo yake kutokana na ubora anaouamini.

Wakati Simba inafanya usajili, kulikuwa na mazungumzo mengi ambayo ninaweza kuyaita ni ya mtaani. Au ni ya kishabiki kwa kuwa wengi waliona Simba ilifanya usajili wa kubahatisha.

Wengi waliona Simba ilichelewa sana kuanza usajili wa wakati Yanga au Azam FC walikuwa wakiendelea kufanya. Huenda hii iliwapa presha mashabiki wa Simba ambao hawakutulia na kutafakari kuhusiana na hilo.

Yanga ina michuano ya kimataifa, lazima isajili mapema. Yanga haikuwa na sababu ya kubadili kikosi chake kwa kiasi kikubwa kwa kuwa kilikwenda kinaimarishwa vizuri na kwa sayansi nzuri kwa misimu mitatu mfululizo na kimeonekana kuwa imara zaidi karibu kila idara.

Hata kama Simba wangetaka kushindana na Yanga, ingekuwa ni watu wawili wenye malengo yanayofanana katika majibu ya mwisho lakini wakati wa utekelezaji ni tofauti sana.

Maneno hayo ya mtaani yamezua maneno Simba imesajili kikosi dhaifu na wachezaji wa bei rahisi. Hii inaweza kuwa ni ya kishabiki sana, lakini inaweza ikabadilika na kuwa sumu hata kwa wachezaji wenyewe kama watakubali iingie masikioni mwao na kuiruhusu izunguke muda mwingi ndani ya ubongo wao.

Simba wanapaswa kuwa makini kwa wachezaji wa kigeni kwa kuwa ni wale ambao hawajawahi kuwaona. Wengi waliowasajili ambao ni wa hapa Tanzania ni wale ambao wamewaona na kuwafuatilia ubora wao, hivyo hawawezi kuwa na sababu ya kuhofia badala yake wachezaji wanapaswa kuonyesha walichonacho au thamani yao.


Narudia, usajili wa Simba si mbaya lakini unaweza kuwa bora kama wachezaji watajitambua na kutaka kuonyesha thamani yao. Unaweza kuonekana hauna lolote ndiyo maana nasisitiza hivi; kama Simba wao wenyewe watakuwa na hofu na kujidharau. Basi mwisho watadharauliwa kwelikweli.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic