July 4, 2016


Kiungo myumbulikaji wa Mtibwa Sugar, Shiza Kichuya anayewaniwa na Simba amefunguka kuwa vimesalia vitu vichache kwa ajili ya kuvaa uzi mwekundu msimu ujao kwa ajili ya kuitumikia Simba.

Kichuya, mchezaji anayesifika kwa mashuti, nguvu na uwezo wa kumiliki mpira, alianza kuhusishwa kuhamia Simba mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Bara, hivi karibuni amefunguka kuwa kwa upande wake tayari ameshamaliza kila kitu na kilichobaki sasa ni uongozi wa Mtibwa kumalizana na Simba.

Aidha, alisema kwamba kwa kuwa bado yupo kwenye mkataba na Mtibwa, kila kitu sasa kimehamia kwa Mkurugenzi wa Mtibwa, Jamal Bayser na yeye ndiye anayefanya mazungumzo ya mwisho na mabosi wa Simba kabla ya kupewa taarifa ya maafikiano ya kumwaga saini.

“Siwezi kulizungumzia kwa undani hili suala lakini niseme tu kwamba kwa upande wangu nishamaliza kila kitu na nimepewa taarifa tu kwamba hata kwa upande wa viongozi wa Mtibwa na Simba nao wamefikia pazuri, kwa hiyo nasubiri taarifa ya mwisho.

“Kimsingi ieleweke kwamba mpira ni ajira yangu na kokote nafanya kazi, kama nitafanikiwa kutua Simba itakuwa safi pia maana popote nitakapokwenda nitapiga mzigo kama kawaida,” alisema Kichuya anayetajwa kuwa moja ya wachezaji walioonyesha kiwango cha juu msimu uliopita.

Kichuya anakumbukwa pia kwa kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi katika Ligi Kuu Bara kwa mwezi Machi katika msimu uliopita ambapo uwezo wake ulimwezesha pia kuitwa katika timu ya taifa kwa mara ya kwanza chini ya Kocha wa Taifa Stars, Charles Mkwasa kwa ajili ya mechi dhidi ya Chad iliyofanyika Machi 23, 2016, jijini N'Djamena.

Kuhusiana na hilo, Bayser alisema: “Tunasikia Simba wanamtaka lakini sisi pia tumepanga kumbakisha kikosini kwetu lakini akikataa hatutakuwa na namna, tutamuacha aende kwani hayo yatakuwa maamuzi yake mwenyewe.”


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV