July 4, 2016




Na Saleh Ally
KARIBU wiki yote iliyopita, gumzo la Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Yanga, Jerry Muro ambaye alitakiwa kufikishwa kwenye kamati ya maadili iliyokuwa inakutana juzi Jumamosi.

Juni 29, mwaka huu, TFF ilimwandikia barua Muro yenye kumbukumbu namba TFF/ADm/LM.47/2016 ikimtaka kuhudhuria katika kamati ambayo ingekutana Jumamosi kujibu mashitaka mawili ya kupingana na maamuzi ya TFF, pia kulishambulia shirikisho hilo kwenye vyombo vya habari.

Kamati ya Maadili ilishindwa kusikiliza shauri la Muro baada ya kuonekana barua aliyoandikiwa haikuwa ikieleza atakwenda kusikilizwa na kamati ipi, licha ya kwamba ya maadili ndiyo ilikuwa inakutana siku hiyo.

Muro ametumia nafasi hiyo kuchomoka kwenye ‘msala’ huo ambao kiundani unaonekana unatokana na ile ishu ya Yanga kuamua kuwaingiza mashabiki wote bure katika mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe, Jumanne iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kipindi hicho, ndicho Muro alionekana kucharuka sana. Aliendelea kueleza msimamo wa Yanga na ambacho hawakukubaliana nacho. Kama unakumbuka wiki chache zilizopita hali ilikuwa hivyo wakati wa ubishani wa uchaguzi wa klabu hiyo usimamiwe na TFF au Yanga na mwisho klabu ikashinda. Mwisho wa uchaguzi, Rais wa TFF, Jamal Malinzi akaipongeza kwa kufanya uchaguzi na kupata viongozi wake!

Safari hii, Muro amechomoka baada ya mwenyekiti wa kamati ya maadili, Wilson Ogunde kuitaka TFF kumuandikia barua nyingine Muro kwa ajili ya kumuita kwenye kamati hiyo.

Ogunde amesema hivyo, kwa kuwa anakiri kweli barua aliyoandikiwa Muro ilikuwa na mapungufu na haukusema anakwenda kuhojiwa na kamati ipi na hapo ndipo ninapoanzia.

Kwamba Katibu Mkuu wa TFF, anashindwa hata kuanzika barua sahihi ya wito wa mtu ambaye anakwenda kwa ajili ya kuhojiwa na kamati fulani. Kwangu naona hiki ni kichekesho cha karne.

Mwesigwa Selestine ndiye mtendaji mkuu wa TFF, baba wa michezo Tanzania! Halafu hata barua moja ya kutoa maelekezo kama hayo, nayo anashindwa kuiandika kwa usahihi. 

Ninaamini atakuwa amendika mwenyewe, ninaamini MWesigwa hawezi kuwa amekopi barua ya zamani na badala yake hiyo iliandikwa upya kabisa kwa ajili ya Muro, lakini imegeuka kichekesho.

Mtuhumiwa kashinda hata kabla ya kuhojiwa kutokana na mapungufu ya msingi ndani ya barua ya taarifa ambayo iliandikwa na katibu mkuu wa shirikisho. Hapa kinachofuata kwa mtu muungwana ilikuwa ni kujiuzulu kwa picha inayoonyesha udhaifu wa juu kabisa.

Binafsi nimejiuliza maswali kibao, kama kweli mtendaji mkuu wa shirikisho anashindwa hilo dogo kabisa ambalo hata katibu muktasi angelifanya bila kupindisha, vipi kuhusiana na umakini wa mambo mazito yanayopita ndani ya shirikisho.

Muro ambaye ni msemaji wa Yanga, anaonekana kuwa makini na mwelewa wa mambo hata kuliko katibu mkuu wa shirikisho! Ameweza kutumia udhaifu wa katibu mkuu kuzuia zoezi la kumhoji, sasa Mwesigwa anatakiwa na kamati kumuita tena, kama akifanya itakuwa aibu nyingine kubwa sana.

Siamini kama TFF inapaswa kumziba kila mtu mdomo, kila anayetaka kujitetea. Ndiyo maana wakati alipofungiwa kimagumashi Dk Damas Ndumbaro niliwaeleza wadau walivyokuwa wakimya wakati watu ‘wananyongwa’ kwa hujuma.

Leo TFF imeshindwa kufikia lengo lake kwa kuwa inafanya mambo kwa jazba. Wote mnakumbuka ilivyoanza kulazimisha kumtuliza Haji Manara wa Simba. Kitu kibaya zaidi, watu wa soka tatizo la msingi ambalo linaonekana si sawa hasa uonevu wa upande mmoja unapotokea, huona ni la upande huo na wanasahau linaweza kurudi kwingine, kama ambavyo safari hii lilivyokuwa linakwenda kuwaangukia Yanga kupitia Muro. 

Vizuri kabisa, Mwesigwa naye angepumzika kwa kuonyesha wazi hawezi kuwa makini kwenye majukumu makubwa ya juu kama ameshindwa kuandika barua tu. Bila viongozi makini hakuna maendeleo katika soka, makosa yanayoonekana madogo, ndiyo makubwa yanayotukwamisha. Tusidanganyane.



2 COMMENTS:

  1. Saleh Ally, km suala lako la kumtaka ajiuzulu kwa makosa ya kiuandishi vipi na wewe ktk makala haya umeyaona makosa haya [MWesigwa]? Au kwa upanga huo huo ujiuzulu?

    ReplyDelete
  2. �������� hivi hiyo ulokosoa imeharibu hoja ya msingi!!?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic