July 1, 2016



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Katika wiki chache zilizopita, kumekuwepo migongano mingi kuhusiana na masuala ya  klabu ya Yanga (Young Africans Sports Club) ambapo haikuwa vyema kuyajibu au kuyajadili wakati klabu hiyo ilikuwa ikikabiliwa na mashindano ya kimataifa.  Lakini kwa hivi sasa ambapo mambo yametulia, nimeona ni wakati mwafaka wa kuyaelezea kama ifuatavyo:

1.     TAARIFA YA MCHEZO KATI YA YANGA NA TP MAZEMBE

1.1.         Ningependa kumshukuru Rais wa Shirikisho la Miguu wa Miguu Tanzania (TFF) ambaye amenipongeza nikiwa kama Rais wa Yanga kutokana na mafanikio yaliyofikiwa na klabu hiyo katika mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika. Hata hivyo, ningependa kuanza kwa kuelezea kwamba mimi Si Rais wa Yanga bali Mwenyekiti, na nikiwa Mwenyekiti wa Yanga, kwa niaba ya klabu hiyo, ninazipokea pongezi hizo.

1.2.         Hata hivyo, pongezi hizo zingepokelewa kwa moyo mkunjufu zaidi na Yanga iwapo TFF ingeisaidia Yanga kama inavyotakiwa kufanya. Mambo ambayo TFF ingeyafanya na kuimarisha utendaji wa klabu hiyo ni pamoja na:

1.2.1.     Kutoingilia ratiba ya ligi kuu mwaka jana ambapo iliiruhusu Azam FC kufanya ziara ambayo ilikuwa nje ya ratiba na hivyo kufanya mabadiliko katika ratiba ya ligi, jambo lililotufanya kushindwa kujipanga vyema.  

1.2.2.     Ingetoa mjumbe wa masuala ya kisheria kutoka TFF kwenda Yanga kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa klabu hiyo uliofanyika huko Angola ambapo ujumbe wetu pamoja na wa vyombo vya habari, ulifanyiwa fujo na kupigwa na polisi wa Angola.  Matokeo yake, badala ya kutuunga mkono katika kupeleka rasmi malalamiko yetu kwenda Shirikio la Soka la Afrika (CAF), TFF lilikaa kimya.

1.2.3.     Ilibidi itupe vifaa vya CAF vilivyotumwa kwa ajili ya kutumika katika hatua za makundi kwa wakati unaotakiwa, jambo ambalo halikufanyika na kutufanya tuingie gharama ambazo hazikuhitajika na kutusababishia adhabu kutoka CAF.

1.2.4.     Ilibidi ichukue hatua kutokana na kuonyeshwa kwa klabu yetu kadi nyingi mno za njano (8) na kadi moja nyekundu katika mchezo wa kundi letu nchini Algeria dhidi ya klabu ya MOB.

 1.2.5.     Ingehakikisha  inatuonyesha wazi tarehe na muda wa mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe ambapo badala yake waratibu waliamua kuupanga mchezo huo dhidi ya TP Mazembe dhidi ya maslahi ya Yanga.  Hali hiyo ilizidi kuvurugwa kwa kufikiwa mkataba wa siri na Azam TV wa kuurusha nchini Tanzania mchezo huo wa Yanga wakati klabu ilikuwa imepiga hatua katika majadiliano  ya shirika la utangazaji ya TBC (ambao mwaka jana walikuwa wamepokea magari matatu kutoka China ili kuimarisha matangazo ya moja kwa moja ambayo yaligharimu kiasi cha Shilingi bilioni 5 kwa kila gari) kwa ajili ya kwa ajili ya kiwango kinachotakiwa katika kurusha matangazo kimataifa.

1.2.6.     Pia ilibidi kuipa Yanga fedha za CAF kwa kufuzu kuingia katika hatua hiyo ya mashindano ambayo ilifahamika kuwa ni Dola 15,000 za Marekani;  fedha za Kombe la FA katika mchezo wake na Azam FC; Zawadi ya VODACOM ya Ligi Kuu, zote hizo zikisemekana kuwa ni kiasi cha Sh. Milioni 500, ambazo iwapo zingelipwa na TFF katika muda mwafaka, Yanga ingezitumia fedha hizo kukabiliana na majukumu mbalimbali ya fedha ikiwa ni pamoja na bonasi za wachezaji hadi usajili wa wachezaji katika dirisha maalum la CAF, na kadhalika.

1.3  Mahali ambapo klabu inasimama leo hii ni kutokana na juhudi zake yenyewe na si kutokana na ushirikiano au msaada wowote ambao Yanga imeupata kutoka  TFF ambapo Yanga kamwe haikuutegemea na ambapo imeona waziwazi kwamba TFF imeshindwa kuisaidia.

1.4 Uamuzi wa Yanga kuwaruhusu mashabiki wa soka kuingia bure katika mchezo huo ili kuweza kumpata mchezaji “halisi japokuwa wa kufikirika” wa 12 si jambo jipya katika soka, japokuwa jambo hilo limekwenda kinyume na matakwa ya TFF ambayo ilitegemea kufanya makato mbalimbali ambayo  yamefutwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).  

Pamoja na hayo yote, kama TFF wanataka kusimamia michezo yetu, basi wachukue gharama zote za maandalizi kabla ya kwenda kwenye michuano kama nauli, posho za wachezaji na kadhalika, hesabu tutawapelekea hivi karibuni. Tunammsihi Rais wa TFF asigeuke kauli yake maana sisi tumewaachia kutafuta fedha kwa ajili ya maandalizi ya mechi zinazokuja kulingana na uzito, tunaamini hatageuka. 

Tunashangaa CAF na TFF walikuwa wapi wakati rais mstaafu Jakaya Kikwete katika mchezo wake wa kwanza katika  Uwanja wa Taifa alipowaruhusu mashabiki kuingia bure?  Inabidi wafahamu pia kwamba tulipocheza huko Angola na Algeria, mashabiki waliruhusiwa kuingia viwanjani bure tulipocheza huko.  Sisi kama klabu tunawathamini mashabiki wetu katika kututia hamasa wakati tunacheza. 

Mimi mwenyewe nilitoa fursa hiyo huko Mwanza miaka ipatayo kumi iliyopita wakati klabu ilicheza dhidi ya El-Merreikh, na hapakuwepo na adhabu yoyote kutoka CAF kutokana na hatua hiyo.  Je, TFF wanatufanyia hivi kama kutuadhibu kutokana na kukosa mapato ambayo yangeliwezesha kufanikisha sikukuu ya Idd el Fitri?

1.5 Uamuzi wa kuwaruhusu mashabiki kuingia bure Uwanja wa Taifa ni jambo lenye busara nyepesi kufahamika kwa mtu yeyote.  Katika mchezo huo ambao ulipigwa uwanjani hapo, mapato yasingezidi Sh. 100 Milioni, na baada ya makato yote ambayo yangehitajika kufanyika, klabu ingejikuta imebaki na kiasi cha Sh. 40 Milioni.  Hii ni kwa kuchukulia kwamba pasingefanyika wizi wowote kwenye milango na pasingekuwepo na tiketi bandia, hali ambayo hufanywa katika michezo ambayo husimamiwa na TFF hasa ile ya ligi.

1.6  Binafsi niliamua kwamba kwa vile Uwanja wa Taifa ulikuwa umekodishwa kwa ajili ya maonyesho ya starehe kwa Sh. 20 Milioni ambapo kwa uelewa wangu  kiasi hicho kilikuwa kimefutwa na Waziri wa Michezo na Utamaduni kwa kuwa Yanga ilikuwa inawakilisha taifa. Klabu iliona ingebeba gharama zingine mbalimbali zenye kuhusika na mchezo huo, yote hayo kwa ajili ya kutaka mashabiki wengi wa Tanzania waingie ili kuitia moyo Yanga katika siku hiyo ya mchezo.

Niliongea na vyombo vya usalama, akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani kuhusu nia hiyo ya Yanga, ambapo  jeshi la polisi lilifanya kazi nzuri sana. Hali ya uwanjani ilikuwa tulivu kabisa isipokuwa nje ambako baadhi ya mashabiki waliuziwa tiketi feki ambazo tunahisi zilikuwa zimetayarishwa na TFF. Hata hivyo, polisi waliweza kudhibiti hali hiyo ambapo hakuna aliyejeruhiwa au kukamatwa, jambo ambalo linaonyesha wazi kwamba woga wa CAF wa kuiadhibu Yanga kutokana na kinachodaiwa vurugu, ni upuuzi mtupu.

1.7  Kuhusu suala la kutakiwa mashabiki  40,000 pekee waingie katika uwanja huo wenye kubeba watu  60,000, jambo ambalo lilizua sababu kutoka CAF kuiadhibu kwa kuipiga faini Yanga, ninashangaa ni busara gani ilitumiwa na serikali katika kujenga uwanja wa kuingiza watu 60,000 na badala yake kutegemea uingize watu 40,000 tu!  

Rais wa TFF hakupewa habari za kweli. Ninachofahamu ni kwamba mratibu wa mechi alisema kwamba maofisa wa TFF walitaka waingie watu 40,000 tu ili kuipunguza nguvu Yanga lakini alikataa, kwani hakuona sababu ya watu kuingia na kuujaza uwanja kama ilivyo kawaida.

Isitoshe,  Kamishna huyo ninaweza kumleta mbele ya Watanzania wasikie jinsi TFF ilivyokuwa inajaribu kumpotosha dhidi ya Yanga kwa vile klabu hiyo ilikuwa imeamua kuionyesha mechi hiyo bure na kuvinyima fursa vituo fulani vya televisheni  kuuonyesha mchezo huo, pamoja na kuvuruga mipango ya TFF ya kupata fedha kutokana na mauzo ya tiketi.  Katika hili, nina fahari kubwa kwa kutoa fursa kwa zaidi ya mashabiki 60,000 kuiona mechi hiyo bure ambayo hata kama hatukushinda lakini tulikuwa pamoja kama Watanzania.

1.8  Nawajulisha wananchi kwamba uhasama kati ya TFF na Yanga si mpya kwani hata katika uchaguzi tuliofanya majuzi, kulikuwa na majaribio ya kutaka kuvuruga matokeo yake, na njama hizi zimefikishwa katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). 

Ni vyema TFF ikashughulikia matatizo yake mbalimbali ikiwa ni pamoja na  kupanga matokeo ya mechi mbalimbali, kuingilia masuala ya klabu mbalimbali kama ilivyofanywa kwa Yanga kwa kujaribu kutumia katiba ya zamani ya mwaka 2010, kuingia mikataba ya siri na wadhamini wa ligi, haki za vituo vya televisheni kuonyesha mechi na kusababisha kuziua klabu kifedha, na  kujifanya kuchukua hatua za maendeleo katika soka kwa unafiki wa kutegemea kodi mbalimbali kutoka Yanga na Simba. 

Sisi katika klabu ya Yanga tuliokuwa katika Kamati ya Utendaji hatuchukui hata posho za vikao kwani tunataka kwanza kuifanya klabu ijitegemee kifedha kabla ya maslahi yetu binafsi.  Kinyume chake, posho ndani ya TFF limekuwa jambo la kawaida, hali ambayo imefanya hata mahesabu yake yasichapishwe kwa ajili ya kupitiwa waziwazi na kila mtu.

1.9 Nasisitiza kwamba katika uchaguzi uliofanyika majuzi, kabla ya hapo nilikuwa Mwenyekiti nikiwa nimechaguliwa kwa kura kwa kipindi cha miaka miwili katika uchaguzi mdogo nikiwa nimeapa kuleta uaminiano kati ya mashabiki na viongozi wa klabu, ambapo kipindi hicho kiliongezwa baadaye kwa mwaka mmoja na wanachama wa klabu, na kuongezwa tena kwa mwaka mmoja kutokana na kufanyika uchaguzi mkuu mwaka jana kutokana na ushauri wa maandishi wa TFF.

Nimesema wazi kufuatia uchaguzi wa majuzi kwamba nitapigania maendeleo  ya klabu kwani hapatakuwa na  cha kufurahia na kuleta amani na utulivu katika klabu iwapo Yanga itashindwa kushiriki katika michuano ya soka barani Afrika, jambo ambalo mashabiki wa Yanga wanalitaka siku zote.

1.10  Pia ninanyoosha mkono wa urafiki kwa klabu ya Simba kwa uchaguzi wao, japokuwa wao hawakufanya hivyo niliposhinda.  Nimeelekeza kwamba utani (ushindani) kati ya Simba na Yanga uwe katika viwanja vya soka, ndiyo maana katika mechi yetu na TP Mazembe niliwakaribisha kama Watanzania wenzetu, tuliwaheshimu wote  pamoja na wale waliovaa majezi na kuishangilia TP Mazembe.

1.11 Mkono huo wa kutakiana mema sitaki ubadilike na kuwa ngumi, bali uendeleze ushirikiano, na TFF iache njama zake dhidi ya Yanga bali iungane nasi katika kujenga soka la Tanzania.


2.     KUITWA KWA JERRY MURRO KATIKA KAMATI YA MAADILI YA TFF AKIWA MKURUGENZI WA HABARI WA KLABU

2.1.         Hati za TFF za kuitwa kwa  Jerry Murro hazionyesha wazi sababu ya Mkurugenzi wa Habari huyo wa Yanga kutakiwa kufanya hivyo ambapo atakuwa akihudhuria si kwa cheo chake katika  klabu, lakini ifahamike wazi kwamba  Yanga haitakubali Mkurugenzi wake wa Habari afungiwe kushiriki katika shughuli za soka. Tukiwa kama klabu  tuko tayari hata kuunga mkono hatua zozote za kisheria dhidi ya TFF na iwapo TFF itajaribu kuifungia Yanga, tutalichukua suala hili hadi katika vyombo vya juu zaidi vya michezo.

2.2.         Hata hivyo, iwapo kuitwa huko kunahusu suala la faini ya Sh. 5 Milioni dhidi ya Jerry, fedha hiyo ilikwishatolewa kwa TFF.

2.3.         Wanaokula njama ndani ya TFF kuwanyamazisha au kuwafungia ambao wanaeleza mawazo yao kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, lazima wafahamu kwamba kuikosoa TFF hakupingani na sheria, na wafahamu pia kwamba Yanga chini ya uenyekiti wangu haitakubali wanachama au wafanyakazi wa klabu kudhalilishwa au kutishwa.

3.     MKATABA WA TBL NA YANGA

3.1.         Mkataba wa kampuni ya bia nchini (TBL) na YANGA ulisainiwa miaka mitano iliyopita na mtangulizi wangu.  Huu ulikuwa mkataba haramu kwani mamlaka ya kutia saini mikataba kwa mujibu wa Katiba ya Yanga yapo kwa wadhamini na hapana kitu kama azimio kutoka  bodi ya wadhamini kuingia katika makubaliano kama haya, au mkataba kusainiwa na wadhamini.

3.2.         Wakati wa kipindi changu kilichopita, nilijitahidi kurekebisha tofauti zote zilizokuwepo, lakini nilishindwa. TBL ni mara moja tu imetoa mara moja tu Sh. 20 Millioni kwa ajili ya tamasha la Yanga Day zilizoahidiwa kutolewa kila mwaka, haijailipa klabu fedha ya marekebisho inayofikia Sh. 30 Milioni wala haijatupa basi kwa kiwango sahihi tulichotaka kama ililoahidi katika mkataba.  TBL imejulishwa kuhusu hili lakini haijalishughulikia.

3.3.         Yanga imeingia katika mkataba wa masoko na kampuni ya International Marketing ili kupata wafadhili wake, ili kupunguza pengo la TBL kwa ajili ya mishahara ya Juni.  Hii ni kampuni ambayo nilikuwa mwenyekiti wake na ikakubali ufadhili huo wa mwezi mmoja, jambo ambalo liliifanya Yanga kuvaa jezi za nembo yake katika mchezo dhidi ya TP Mazambe.

3.4.         Iwapo wanachama wa Yanga wakihisi nilivunja katiba kwa maslahi yangu binafsi au wakiwa na sehemu nyingine bora zaidi ya kufanya hivyo, walifikishe suala hilo kwenye kamati ya maadili ya klabu kwa ajili ya uamuzi.

4.     MUHTASARI

4.1.         Nimechaguliwa katika mazingira ya amani zaidi miongoni mwa vyama vya soka nchini na ambapo hakuna hata senti moja ilitumika kwa ajili ya kumhonga yeyote.

4.2.         Nilisimama bila kupingwa kugombea nafasi ya Mwenyekiti na nikawaambia wapiga kura wangu waziwazi kwamba: Wakati huu nikiwa Mwenyekiti sitakaa kimya kwa wale watakaojikita katika kuhujumu masuala ya fedha klabuni na wale wanaoamini kwamba TFF iko juu ya sheria zinazohusu masuala ya biashara na haihusiki na Katiba ya Tanzania.  Nawashukuru wapiga kura wangu ambao walinipigia kura kwa asilimia 100 ya ushindi wangu.

4.3.         Masuala yanayotokea uwanjani au usajili wa wachezaji ni ya soka na kwamba TFF ina mamlaka ya  kuipeleka mbele nchi yetu kwa kufuata miongozo ya FIFA.  Lakini sitavumilia upuuzi wa TFF kutaka kuingilia masuala ya Yanga.  Tunajua FIFA imechafuka kwa rushwa na kusababisha Sepp Blatter kuong’olewa na kukabiliwa na mashitaka: hata hivyo, iwapo tungetumia kauli za TFF, Blatter na Platini wasingefanywa chochote.

Masuala ya fedha ya klabu yetu, yawe kuhusu nembo ya klabu kwenye kituo cha televisheni bila ya kibali cha Yanga si ya kuamuliwa na TFF.  Kilichopo ni kwamba  kitu cha televisheni kinatengeneza fedha kutoka kwa Yanga, TFF inatengeneza fedha kutoka kituo cha televisheni.  Hivyo, iwapo kuna mtu anafikiri sijui sheria za mashindano  bora ya kibiashara na hakimiliki, basi wajue hilo litawagharimu.

4.4.         Iwapo TFF inataka Mwenyekiti wa Yanga akubaliane na uwongo, basi katika miaka minne ijayo niko tayari kupambana na uovu huo na kusahihisha kila kitu.    Hata hivyo, kwanza kabisa niko tayari  kushirikiana kirafiki  na wakati huohuo kupigania haki za klabu kwani daima nimekuwa mtu mwenye kupigania haki na masuala ya kikanuni ninayoyaamini ni ya kiadilifu.

4.5.         Yanga ilikuwepo kabla yangu na itakuwapo baada yangu.  Ni wajibu wangu kuiacha Yanga ikiwa klabu bora zaidi kuliko nilivyoikuta na nikiona siwezi tena kutumikia maslahi ya wanachama wake, sitasita kujiuzulu au kuitisha uchaguzi ili kujipanga upya.

5.     MWISHO:

5.1.         Kwa mashabiki wa soka wa Yanga na Tanzania nzima, tumefikia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho si kwa bahati. Mwaka jana tulitolewa kwa tofauti ya mabao ya kufunga.  Na mwaka huu tumekutana na uhasama katika mechi zetu ambapo tulipigwa mabomu ya machozi, mbali na huko Misri ambako tulifanyiwa njama mbalimbali.  Vilevile TFF nayo imekuwa haitupi msaada wowote bali kutuhujumu tena.  Nasema sitavumilia hujuma hizi dhidi ya Yanga.

5.2.         Sisi ni klabu ambayo tumejaa ujasiri, hatujalipiza kisasi kwa tulichofanyiwa wapinzani wetu wakija hapa.  Ndiyo, tumeshindwa mechi mbili, lakini kwa heshima.

Hatutashusha vichwa vyetu kwa aibu au kutaka kufanikisha mambo yetu kwa njia za panya. Tutawekeza katika timu yetu kila raslimali.

Natoa wito kwa Yanga kutokata tama katika juhudi za kujenga uwanja wetu juu ya misingi aliyoiacha Mzee Karume.

Tusisahau kwamba tulikuwa msingi wa nguvu zilizomfanya Mwalimu Nyerere kuikomboa Tanzania na nchi nyingi za Afrika.
Historia yetu imejaa kila aina ya fahari.

Tumepigania yote tuliyoyaamini na tumeshinda.

Matumaini yetu ya kutwaa kombe la ushindi wa ubingwa katika Afrika yako karibu na kwamba kila hatua tufanyayo inatupeleka karibu na lengo hilo.

Mustakabali wetu unatuonyesha kwamba kama si mwaka huu, basi mnamo miaka mitatu ijayo tutafika katika fainali za michuano hii tukishirikiana vyema.

Ni kweli wasaliti wapo, lakini lazima tusonge mbele, kila tunapokatishwa na tama na watu wengine, basi tujue tunakaribia ushindi wetu.

5.3.         Nataka kila mtu aamini kwamba hii ni timu yake si yangu mimi.  Tunamtaka zaidi kila mtu hivi sasa kwani tunakaribia katika lengo letu la kutwaa ubingwa wa Afrika, japokuwa tunafahamu kwamba kuna mengi ya kufanya lakini mengi zaidi tumeishamaliza, kikubwa matunda yanaonekana na tunashiriki michuano ya kimataifa tunashiriki na tunapiga hatua moja mbele.

5.4.         Si rahisi lakini tusilalamike. Hakuna kitu Mungu anatuwekea mbele yetu bila ya sisi kuwa na nguvu ya kuvuka. Kwa imani, DAIMA MBELE, NYUMA MWIKO.
Asante.
(YUSUF MEHBUB MANJI)
MWENYEKITI WA KLABU YA YANGA 


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic