July 13, 2016


Wanachama na mashabiki wa Yanga, leo hii wanatarajia kumkabidhi fedha za matibabu Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara ambaye anasumbuliwa na matatizo ya macho kabla ya kuondoka kwenda zake nchini India kwa ajili ya matibabu.

Manara alikumbwa na hali hiyo hivi karibuni jambo ambalo limesababisha jicho lake la kushoto kutoona kabisa lakini pia lile la kulia nalo linadaiwa kupunguza uwezo wake wa kuona kama ilivyokuwa zamani.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga zimedai kuwa baada ya wanachama pamoja na mashabiki wa timu hiyo kuchangishana fedha hizo kwa zaidi ya wiki moja wanatarajia kumkabidhi leo hii.

Hata hivyo haikuweza kujulikana mara moja kuwa ni kiasi gani lakini kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Habari wa Yanga, Jerry Muro hivi karibuni aliliambia gazeti hili kuwa kiasi watakachomkabidhi kitakuwa zaidi ya Sh 1,000,000.


“Tumeshakusanya fedha nyingi sana na kesho (leo) tutamkabidhi Manara mchango wetu huo ili aweze kuongezea katika harakati zake za matibabu,” alisema mtoa habari huyo ambaye ni mmoja kati ya waratibu wa zoezi hilo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV