August 6, 2016Kikosi cha Simba, jana asubuhi kilifanya mazoezi yake kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam baada ya juzi Alhamisi kurejea kikitokea Morogoro kilipokuwa kimepiga kambi yake ya takriban mwezi mmoja kujiandaa na Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Katika mazoezi hayo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Boko Veterani jijini hapa, wachezaji wa timu hiyo walionekana kuwa wapo fiti kutokana na jinsi walivyokuwa wakipambana uwanjani takriban saa mbili bila ya kuchoka huku wakionyesha uwezo wa juu wa kukaba na kutengeneza nafasi za kufunga.


Kutokana na hali hiyo kocha mkuu wa timu hiyo, Mcameroon, Joseph, Omog amesema, safari hii ubingwa ni mali yao, hivyo wapinzani wao wataisoma namba na amejipanga kuuchukua bila ya kupoteza mchezo wowote kama alivyofanya wakati akiifundisha Azam FC.

 “Nashukuru Mungu tunaendelea vizuri na mazoezi yetu, lengo letu kubwa ni kuhakikisha tunaibuka mabingwa.


“Vijana kama ulivyowaona wapo fiti na tayari kabisa kwa mapambano hata kama wakisema ligi ianze leo kwani tulipokuwa Morogoro nilijitahidi sana kuwajengea stamina na uwezo wa kucheza kitimu ndiyo maana wanaonekana kuwa fiti.

"Kilichobakia sasa ni kuwaongezea vitu vichache tu vya kiufundi na baadaye ni kutafuta ushindi tu kwa kila mechi. Simba ya safari hii ni tofauti na ya msimu uliopita,” alisema Omog akiungwa mkono na msaidizi wake, Mganda, Jackson Mayanja.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV