Na Saleh Ally
MJI wa Shinyanga umekuwa na timu kadhaa za soka kuanzia miaka ya 1980, Mwadui FC ndiyo ilikuwa bora zaidi hadi iliporejea miaka mitatu iliyopita.
Baadaye ilikuwa ni RTC Shinyanga iliyobadilishwa kuwa Biashara pia Shinyanga Shooting. Hizi ndiyo timu zilizotamba kwenye Ligi Kuu Bara na pia kuifanya timu ya mkoa ‘Igembe Nsabo’ kuwa moja ya timu bora kabisa.
Wakati huo, wachezaji wengi wamepita Shinyanga lakini si rahisi kuwasahau kama Nassib Abbas ‘Babu’, Mwinyimvua Komba au Masolwa, Edibily Lunyamila, marehemu Alfred Kategile na wengine wengi.
Kwa sasa fahari ya Shinyanga inaanzia kwa Stand United ingawa kuna Mwadui FC ambayo inatokea nje ya Mji wa Shinyanga wakati Stand United ndiyo watoto wa mjini hasa.
Stand United iko hapo kwa akili za wapiga debe wa mabasi ambao ofisini kwao ni stendi na wanalazimika kupiga kelele ili kuita wateja waweze kuingiza ujira wao kwa siku.
Hawa watu, walipaswa kupewa shukurani kubwa na Wanashinyanga kwa kuwa kwa akili zao ambazo sasa zinaonekana ni ndogo au hazifai, waliiwezesha Shinyanga kurejea kwenye ramani ya soka Tanzania baada ya kuipandisha timu nyingine mpya kabisa katika ramani ya soka ikiwa si Mwadui FC, RTC, Shinyanga Shooting au Biashara. Pongezi kubwa kwao.
Wakati wao wanaipandisha pamoja na kuwa masikini, hata matajiri wa Mwadui ambako ni machimbo pekee makubwa ya madini ya Almasi, hawakuwa wameweza kufanya hivyo.
Stand United ilianzishwa mwaka 2011, ikasajiliwa rasmi Januari 24, 2012 ikiwa na wanachama 33 ambao wote ni wauza tiketi au wapiga debe wa mabasi ya Mombasa Raha, Mohamed Trans na Ally’s ya mkoani humo. Wakati huo, hakuna kiongozi wa Chama cha Soka Shinyanga (Shidifa) aliyeamini watu hao wangefika mbali hadi kucheza Ligi Kuu Bara.
Hakukuwa na kiongozi hata mmoja kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambaye aliwapa hata mawazo kuwasaidia kusonga au aliyejua wangepata udhamini wa Kampuni ya Mgodi wa Acacia ambayo ilikubali kutoa hadi Sh bilioni 1.2 kwa mwaka na kuifanya Stand kuwa timu yenye mkataba mkubwa zaidi hata kuliko Yanga na Simba. Mkataba huo, ndiyo ulioanzisha matatizo hadi kufikia timu hiyo kuondolewa kwa nguvu, kidhuluma kutoka mikononi mwa wanachama sahihi, wamiliki sahihi hadi kwa watu waliokimbilia kupata fedha.
Kisa kimeanza kuwa madai ni wapiga debe, wanaonekana si wasomi na fedha ni nyingi wasingeweza kuendesha timu. Ndiyo maana watu walipandikizwa wakiamini sasa wana akili nyingi na uwezo wa kuendesha klabu na timu eti kwa kuwa kuna udhamini mkubwa.
Watu wa Stand United wangeweza kuajiri wataalamu kwa ajili ya kuendesha timu yao. Kamwe haijawahi kutokea ukasikia mmiliki wa timu anafanya kazi zote.
Najiuliza, vipi wa Shidifa na TFF wamekubali timu hiyo ipokwe mikononi mwa watu wa Stand United ambao wanajulikana mbele yao na hata Wanashinyanga wote kuwa ndiyo wamiliki wa timu hiyo.
Vipi Shidifa na TFF, ndani yake kuna baadhi ya viongozi wake walishiriki mchakato wa uhamishaji wa timu hiyo kwenda kwenye mikono mingine. Aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga, naye alihusika hadi kuunda kamati na niseme hivi, yeye hakuwa mtu mwenye uchungu na Stand United kwa kuwa ni mgeni mkoani Shinyanga.
Sasa inatia hofu kubwa kama vijana au makundi ya wajasiriamali wanaoweza kuanzisha timu, zikifanikiwa na kupata udhamini mkubwa. Wenye akili zaidi ambao hawakuwa na mawazo ya kuanza mwanzo ndiyo wanaona wanaweza kushikilia na kuendesha.
Tayari kuna taarifa ya uchotwaji fedha kwenye akaunti za Stand United na huenda fedha za udhamini wa Acacia zikaanza kutumika vibaya na kuwafaidisha watu hao wasio na uchungu na Stand United na badala yake wenye hamu ya kuzigawana fedha hizo.
Mmoja wa viongozi wa zamani wa TFF, naye yumo kama ‘mshenga’ lakini naye aliona baada ya ushenga, basi aingie kwenye kundi la waendesha klabu. Jiulize Stand United ingekuwa haina fedha, nani angeililia au kuigombea? Nani angeona vijana wapiga debe hawana uwezo tena na vipi vyama vyenye nguvu ya kupigania mpira viingie na kuchukua haki bila ya kuzuiwa?
Harufu ya tamaa, ukabila, uzandiki, uzuzu na tamaa kichaa ndiyo imepitisha dhuluma ya wazi kutoka kwa wanyonge waliotumia akili zao kuanzisha na kukisimamisha kitu. Sasa wamepokonywa mbele ya hadhara ya Watanzania wote na serikali ipo.
Nani asiyejua kuwa wale ndiyo wahusika wakuu na waliopo sasa wamefanya dhuluma huku waongoza mpira kama TFF na Shidifa wakiwepo na wasiseme lolote? Hii maana yake, itafikia siku Mbao FC, wale mafundi selemala, nao wataonekana hawafai na timu yao itakwenda mikononi kwa wanaoonekana wana akili sana?
Serikali haina nguvu mbele ya TFF? Serikali haina ujanja mbele ya Shidifa? Je, serikali haijui kama hii ni dhuluma na kwa nini Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ambaye alionekana mpigania haki za wanamichezo na wasanii kwa nini amekaa kimya?
Ninaamini suala hili linahitaji uchunguzi zaidi na kufuatiliwa kwa undani. Serikali isikubali maneno ya wajanja wanaoona makondakta hawafai kwa kuwa tu eti hawajasoma au si watu wanaoweza kuendesha klabu ambayo ina udhamini mkubwa. Hii si kweli, hii ni dhuluma.
Kamwe haitakuwa sawa hata kidogo kama Watanzania wa maisha ya kiwango cha chini wataendelea kudhulumiwa na wale wanaojiona wana nafuu ya kimaisha. Vyombo husika vipo na serikali ipo na zoezi la dhuluma lifanikiwe, hii si sawa.
Chondechonde serikali, onyesheni nyie ni wazazi na warekebishaji, haki ilipopotea. Hawa makondakta wanadhulumiwa mbele ya umma wa Watanzania.
Hili lisikubaliwe liendelee haiwezekani wakati Waziri yupo likipita tutajua na yeye anahusika katika huo uporaji wa Haki.
ReplyDeleteBig Up Salehe mawazo yako ni ya kujenga tusaidie wahusika walipate na tupate majibu.