August 10, 2016


RAIS WA TFF, JAMAL MALINZI

Na Saleh Ally
UNAPOSIKIA mazungumzo yanahusisha ligi katika soka, zaidi unategemea mwenendo wa uwanjani na mafanikio yake.
Soka ya Tanzania, ilianza kubadilika mwanzoni mwa miaka ya 1990. Kabla ya hapo, Chama cha Soka Tanzania (Fat), kiliongoza malumbano na soka likawa maarufu sana kwenye midomo na maofisini.

Suala la nani anachezaje, takwimu zipi ni bora, lilikuwa chini kwa kuwa Fat, hata viongozi wake, Mwenyekiti Muhidin Ndolanga na katibu wake mkuu, Ismail Aden Rage walikuwa hawaelewani na malumbano yalikuwa juu. Kila mmoja, alikuwa kundi lake ambalo lisingefurahi mwingine kushinda.

Hali hii, ilisababisha suala la malumbano kuwa juu zaidi na maarufu kuliko mpira wenyewe. Kipindi hicho, hata timu ya taifa, Taifa Stars ilikuwa ikilala kwenye hosteli za Jeshi la Wokovu. Ninaamini zingekuwepo leo, hata timu za daraja la kwanza, zisingekubali kuweka kambi pale.

Malumbano bila kwisha ndani ya Fat, yalifanya mpira kutawaliwa na maneno zaidi kuliko vitendo. Hali hii sasa inaonekana kurejea kwa kasi zaidi na kutoelewana kwa waziwazi kati ya Yanga na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kunachukua nafasi kubwa kabisa.

TFF chini ya Jamal Malinzi, huenda imeshuka chini ya Fat kwa maana ya maendeleo. Pia unaweza kusema imefeli zaidi maana licha ya kuwa na wadhamini wanaotoa mamilioni ya fedha, Taifa Stars haijawahi kwenda hatua ya juu kimafanikio na kupita ile ya enzi za Fat ambayo viongozi wake walikuwa hawana wadhamini kama walionao TFF sasa.

Huenda TFF, ilitakiwa itumie muda mwingi kufanya mipango ya maendeleo kuliko kuwa walumbanaji wakubwa na Yanga, utafikiri nao ni wawakilishi wa timu fulani. Au utafikiri vijana wakizozana kuhusiana na yupi bora katika waigizaji filamu za ubabe, Anold Shwarzenegger ‘Shozniga’ na Sylvester Stallone maarufu kama Rambo.

MWENYEKITI WA YANGA, YUSUF MANJI AKIWA NA BAADHI YA WANACHAMA.

TFF ilitumia nguvu nyingi kuonyesha Yanga imekosea kuingiza watu bure katika mechi dhidi ya TP Mazembe. Ikaandika barua ikiwa ni pamoja na kuainisha kwamba kuna uharibifu, kuna fedha zinatakiwa zilipwe kwenda serikalini pia Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA).

Siku chache baadaye, serikali ikasema tofauti, siku chache tena TRA ikaibuka na kusema kama hakuna mapato, hakuna kodi ya kulipwa. TFF ikakaa kimya na kuumbuka.

Hivi karibuni, TFF imeibuka na suala la Yanga kutotuma majina kwenye Mtandao wa Uhamisho wa Kimataifa (TMS). Tena inataka kuona utetezi wa Yanga kwenda Fifa au ishushwe hadi daraja la tatu.

TFF ni mzazi, Yanga haikutuma, kabla kuna chochote kilifanyika kwa maana ya kukumbusha au kuwataarifu? TFF ni msimamizi wa masuala ya mpira, isikae pembeni kusubiri timu ikosee na yenyewe isimamie adhabu, kwani ikikumbusha kama msimamizi wa mpira ingepata hasara gani?

TFF wametoka kumfungia Msemaji wa Yanga, Jerry Muro bila kufuata taratibu sahihi. Hakupewa nafasi ya kujieleza, alipewa wito umekosewa, akaenda na kuwakosoa. Aliposafiri, nyuma yake wakatuma mwaliko.

Yanga wameendelea nao kutunisha msuli wakitaka kuonyesha hawana hofu na watapambana. Huenda kukosea kila mara kwa TFF kunawafanya wapate nafasi ya kusema pia.

Huenda Yanga pia wanaamini wana nguvu. Nimesikia hivi karibuni kuna mpango wa mechi zote za Ligi Kuu Bara kuwa bure! Unajiuliza vipi? Yanga wamejibu kuwa mechi hazina watazamaji, wakiingia watu wengi wanaingiza angalau Sh milioni 3 tu.

MASHABIKI NA WANACHAMA WA YANGA, WANGEPENDA KUONA TIMU YAO INATENDEWA HAKI. TFF INAPASWA KUKUMBUKA, HAWA WANA NGUVU YAO NA WAO NDIYO WANAIFANYA IJIENDESHE KWA KUWA HAINA MTAJI WA KUUZA MAFUTA WALA KUTENGENEZA MATOFALI. TFF INATEGEMEA SOKA NA HAINA TIMU YA SOKA, HIVYO INAPASWA KUZIHESHIMU KLABU NA KUZITENDEA HAKI.

Hivyo wanaona, bora kupata mashabiki wengi zaidi waishangilie timu na kushinda kuliko kuingiza fedha kiduchu ambazo wakati mwingine hazifikii hata robo ya zile walizotumia kwenye maandalizi ya mechi moja tu!

TFF inayachukulia mambo mengi kwa jazba na mwisho inaonekana kuwa mpinzani mkubwa wa Yanga ambayo ni timu na wao ni shirikisho. Haliwezi kuwa jambo sahihi hata kidogo.

Inawezekana TFF ina nguvu kisheria katika soka nchini. Lakini wao hawana timu, hakuna anayekwenda uwanjani kuiona TFF ikicheza. Lazima ithamini michango ya klabu ambazo zinagharimia timu zao na kuifanya TFF kuingiza fedha.

TFF haina gharama ya maandalizi ya timu, ikiwa na gharama za uendeshaji ofisi, inategemea timu zicheze, ipate fedha. Inategemea wadhamini kupitia timu, inategemea fedha kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), lakini bado yenyewe ni tegemezi tu.

Kuna kila sababu kuwa na viongozi wenye busara na wanaoweza kuufanya mchezo wa soka usiwe sehemu ya chuki au sehemu ya wao kuonyesha wana madaraka, wanaweza kufanya wanachotaka bila ya hofu.

Kwangu nashangazwa sana kuona Yanga ikizozana sana na TFF. Mara nyingi najiuliza, Rais wa TFF, Jamal Malinzi na katibu wake, Mwesigwa Selestine, wote wamekuwa makatibu wakuu wa Yanga kwa nyakati tofauti! Sasa vipi wako kwenye mgogoro na Yanga na kila kukicha unaanza mwingine?

Wakati wakiwa Yanga hawakutendewa haki, wana hasira sana? Au waliahidi wakipata nafasi sehemu nyingine Yanga itawakoma?

Lakini najiuliza pia, kama ni Yanga pekee, msimu uliopita Simba walilalama sana kuhusiana na TFF. Tunajua walikuwa na hoja nyingi za msingi zikiwemo kuhusiana na kamati ambazo mimi naziona zipo kutetea maslahi ya viongozi wa TFF.

Hassan Kessy alipopigwa na Donald Ngoma na mengine mengi, bado walikaa kimya, lakini inapofikia wanataka wao kumfungia mtu, wiki moja haipiti, kikao kinaitishwa na mara moja mtu anafungiwa.

Tunataka demokrasia kwenye masuala ya siasa, itakuwa kichekesho sana kama soka litaendeshwa na vioja, ujeuri, kujidai kutoogopa, chuki na ubabe usiokuwa na sababu za msingi.

Viongozi wa Yanga na TFF, lazima wajue busara ni namba moja kwa kuwa wanaongoza watu ambao wanategemea kuwaona wao zaidi wanafanya mambo ya maendeleo kuliko malumbano ya kijinga kama yanayoendelea sasa.

Yanga na TFF ni sehemu ya historia ya mpira wa Tanzania. Hatuwezi kuwa na maendeleo tukiwa na historia inayokinzana kila kukicha.

Achaneni na mambo yasiyo na faida kwenye mpira wetu. Kutaneni na kumaliza haya yasiyo na faida lakini bado niwasisitize TFF, viongozi mliopewa dhamana, mistake kuligeuza shirikisho kama ni mali yenu binafsi, wengi walishindwa na leo hawapo hapo. 

Tendeni haki muwapunguzie Watanzania wapenda soka suala la kuendelea kumkumbuka Leodegar Tenga na kujuta kwa nini mliingia madakarani. Chonde, usaidieni mpira wetu, maana hautafaidika na malumbano badala yake, mipango na malengo.



5 COMMENTS:

  1. Una hoja ila kuna mambo hujiweka sawa. Kwa mfano suala la usajili hujaonyesha kwamba TFF haikuwasiliana na Yanga au la? Pili suala la mechi kuruka live na kupungua kwa mashabiki ni kweli ila lazima tutambue kwamba timu karne hii haiwezi kutegemea mapato ya mlangoni pekee.Timu ina mdhamini mmoja lazima iwe hasara kwao. Mwisho tukubali uweledi umepungua katika taasisi za michezo za Tanzania.

    ReplyDelete
  2. NDUGU mimi si shabiki wa yanga wala TFF lakini mengine tunawakosea TFF. MFANO, Yanga hawajapeleka majina TFF CHAKUWALAUMU TFF NI KIPI? Mbona yanga tu wakati wamesema hata COASTAL UNION hawajapeleka?

    Yanga wameitwa kwenye semina elekezi hawajaenda, PIA kwenye TMS hawajaingiza majina sasa hao TFF hayo majina wayatoe wapi? je wapeleke waliyo nayo wanayoshiriki shirikisho? Je yanga wakisema hao tumewatema kwa msimu ujao tumesajiri wengine? pia system ilikuwa on had saa 6:00 usiku na wangeweza kuingiza muda wowote hadi saa 5:59 sasa TFF wakawatafute wapi watu amabao wanajuwa kila kitu ndio maana hawakwenda kwenye semina elekezi, Mimi nafuatilia sana michezo na TFF WAMETANGAZA SANA, SANA TENA SANA KWAMBA JAMANI SAFARI HII HATUTAONGEZA MUDA, WAMEVIKUMBUSHA VILABU KILA SIKU KWENYE VYOMBO VYA HABARI. Tuwalaumu kwa mengine wanapokosea ila siyo kuendekeza ujivuni wa watu wachache kuwabebesha lawama TFF. NINGESHAURI ANZA KWANZA NA YANGA WAULIZE KWANINI HAMKUINGIZA MAJINA KWENYE SYSTEM? WAULIZE TFF KWAMBA YANGA WAMESEMA WALIFANYA MOJA MBILI TATU KWANINI NYIE TFF HAMKUFANYA NA NYIE KWA SEHEMU YENU? UKIONA WANALEGA NDIPO UWALAUMU TFF KAMA UTARIDHIKA NA MAJIBU YA YANGA

    ReplyDelete
  3. Saleh huwa naheshimu sana Blog yako kiasi ambacho huwa silali bila kuifungua ili kupata Habari. Lakini katika Makala hii kwa kweli haijakaa sawa na umejaribu kupotosha Ukweli kwa maslahi ya Yanga ambayo hayataisaidia sana timu hio zaidi ya kuingamiza.Ni bora usimame kwenye kweli ili mhusika ajue haendi katika njia iliyonyooka kwa mfano Usajili wa TMC ambao sasa unaigharimu Yanga

    ReplyDelete
  4. Saleh huwa naheshimu sana Blog yako kiasi ambacho huwa silali bila kuifungua ili kupata Habari. Lakini katika Makala hii kwa kweli haijakaa sawa na umejaribu kupotosha Ukweli kwa maslahi ya Yanga ambayo hayataisaidia sana timu hio zaidi ya kuingamiza.Ni bora usimame kwenye kweli ili mhusika ajue haendi katika njia iliyonyooka kwa mfano Usajili wa TMC ambao sasa unaigharimu Yanga

    ReplyDelete
  5. OFA ZA YANGA NA SIMBA – NANI NANI KALA, NANI KALIWA?
    1). KLABU YA SIMBA KUMUUZIA MOHAMMED DEWJI ASILIMIA 51 YA HISA ZOTE:
    a). Simba inapaswa kujigeuza na kuwa Kampuni ya Umma ya Hisa
    b). Thamani ya Hisa shilingi Bilioni 39
    c). Kama Mohemmed Dewji akiwekeza shilingi Bilioni 20 sawa na asilimia 51
    d). Wanachama waliobakia wataambulia shilingi Bilioni 19 sawa na asilimia 49.
    e). Dhana ya Simba kuwa Klabu ya Wanachama itakuwa haipo
    f). Kununua Hisa katika Klabu ya Simba itakuwa wazi kwa kila mtu
    g). Vikao vyote vitafanyika kwa mujibu wa katiba ya Kampuni chini ya Bodi

    SWALI GUMU LA KUJIULIZA (..?..)
    Je Simba itakuwa na thamani isiyozidi shilingi Bilioni 39 – Jina la Klabu, Nembo, Timu, Viwanja, Majengo, Mamilioni ya Wapenzi na Mashabiki Tanzania na Afrika ya Mashariki yote (Fans-base) na Assets zake?

    2). KLABU YA YANGA KUMKODISHIA YUSUF MANJI TIMU NA NEMBO KWA MIAKA 10:
    a). Yanga inabakia kuwa Klabu ya Wanachama wenye mapenzi na Yanga
    b). Yusuf Manji kuichukia Timu na Nembo kisha kuifanyia biashara faida zake:
    - Gharama za uendeshaji wa Klabu zitakuwa ndogo au hazipo kabisa
    - Klabu haitakuwa na matatizo ya aina yoyote juu ya uenseshaji wa timu
    - Klabu itakuwa ikipata mgao wake wa 25% kutokana na faida itakayopatikana
    c). Klabu na Wanachama watakuwa huru kuingia mikataba na wabia wengine watakaojotokeza kuwekeza kwenye kuazisha Televisheni ya Yanga, Kujenga Kiwanja cha mashindano, Kujenga hosteli, Kufungua biashara za faida kwa jina la Klabu, nk kama atakavyofanya Yusuf Manji anapotaka kuichukua / Kuikodisha Timu na Nembo tu.

    SWALI LA KUJIULIZA (..?..)
    Jina la Klabu, Nembo, Timu, Viwanja, Majengo ya Janwani na Mafia, Mamilioni ya Wapenzi na Mashabiki Tanzania na Afrika ya Mashariki yote (Fans-base) na Assets zake zina thamani gani?

    MAONI YANGU: Klabu ya Yanga itakuwa kwenye mazingira bora na salama katika zoezi zima la kumpatia / kumkodishia Yusuf Manji – timu na nembo (si klabu nzima), alimradi pande zote mbili (yaani Yusuf Manji na Bodi ya Udhamini kwa pamoja) ziweke maslahi ya kusaidia Klabu ya Yanga na kuondoa dhana ya kujitajirisha mtu binafsi katika mkataba huo.

    Hivyo wanachama wa vilabu hivi viwili ndiyo wenye kauli ya mwisho kuwapa au hapana.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic