September 14, 2016

Baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe kumkabidhi zawadi ya gari beki wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye sasa anajulikana kama Zimbwe Jr, mengi yameibuka ikielezwa kuwa zawadi hiyo ni kama ushawishi wa Simba kumtuliza mchezaji huyo asisaini mkataba kwa wapinzani wao, Yanga.

Taarifa hiyo imekanushwa vikali na Hans Poppe akidai kuwa hawezi kufanya hivyo na kwamba hayo ni maamuzi yake mwenyewe hawezi kumuingilia na hata zawadi hiyo ameitoa kama mtu binafsi mpenzi wa Simba na si kwa cheo cha uongozi. 


Kabla ya zawadi hiyo, tayari ilishavuja ikidaiwa kuwa Tshabalala ni mmoja wa wachezaji wanaowaniwa na Yanga na kwamba kuna mazungumzo yalishafanyika kuhusiana na kuhamia Jangwani mapema atakapomaliza mkataba wake Msimbazi.

Katika ufafanuzi wake alipokuwa akizungumza na Championi Jumatano, Hans Poppe alieleza kuwa hata kuhusu ishu ya kumpa mkataba mpya atakapomaliza alionao sasa, tayari walishazungumza naye na wameshakubaliana, hivyo hawana sababu ya kutumia nguvu kubwa kumshawishi zaidi ya maongezi hayo ya awali.

“Hapana, siyo kweli kwamba ile gari ni ishu ya ushawishi kuhusu mustakabali wa mkataba wake mpya. Ile gari nimempa kama zawadi tena si zawadi kutoka Simba, ni zawadi kutoka kwangu nikiwa kama mtu binafsi baada ya kuridhishwa na uwezo na mchango wake akiwa Simba.

“Siwezi kumzuia kama anataka kwenda kwingine, tumesikia kuna timu fulani inamtaka na hiyo ni kwa kuwa ni mchezaji mzuri, wanamletea tamaa lakini ifahamike kuwa bado ni mchezaji wetu, ana mwaka mmoja na tumeshazungumza, tumekubaliana kuwa ataongeza miaka mingine mitatu.”

Alipoulizwa kuhusiana na ishu ya zawadi ya gari kwa mchezaji bora wa msimu wa timu hiyo kama ilivyoahidiwa na uongozi huo hapo awali, Poppe alisema: “Hiyo bado sijafahamu inakuwaje, ni suala la timu, si binafsi kama hili na pengine niseme tu kuwa kama kuna mchezaji mwingine atafanya vizuri kama Tshabalala basi naye atapata gari, hata wiki ijayo ikitegemea na kiwango chake.”
Upande wa Tshabalala kuhusiana na ishu hizo alieleza hivi: “Nishukuru tu kwa hii zawadi ambayo imepatikana kutokana na juhudi zangu, upande mwingine inaniongezea morali ya kupambana zaidi na ili nipate vingine zaidi ya hivi na kufika mbali zaidi ya hapa.

“Kuhusu makubaliano ya hili gari na ishu za mkataba wangu hilo siwezi kuelezea chochote, meneja wangu ndiye anayeweza kulitolea ufafanuzi mzuri zaidi.”

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV