September 14, 2016

Simba inatarajia kujitupa dimbani tena Jumamosi ya wiki hii kuumana na Azam FC lakini tayari imegundua ni sekta gani Azam wanaweza kuitumia kuwazidi ujanja, hivyo tayari imejipanga kuhusiana na hilo.

Simba imejinadi kuwa itapambana na timu hiyo kusaka ushindi kwa udi na uvumba lakini imebaini kuwa Azam inaweza ikabebwa kwa kutumia faida ya nyasi za bandia zilizopo katika Uwanja wa Uhuru, Dar watakaoutumia katika mchezo huo.
 Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, amefafanua kuwa wanafahamu ugumu wa mechi hiyo kutokana na sababu ya kung’anga’nia kukaa kileleni, hivyo itakuwa kama fainali ingawa wanahisi wapinzani wao watakuwa na faida na nyasi za uwanja, hivyo nao wanajua wafanye nini siku hiyo.

“Mechi itakuwa ngumu, wote tuna pointi 10 na tuna idadi sawa ya mabao ya kufunga na kufungwa. Wao wanahitaji ushindi kama ilivyo kwetu tunavyouhitaji kwa nguvu zote. Tunafahamu pia wao wamezoea nyasi bandia, tofauti na sisi, hivyo hicho kinaweza kuwa kikwazo kwetu.

“Lakini kama benchi la ufundi tunajua tutafanya nini na hakuna kitakachoharibika, tutalizingatia hilo katika mazoezi yetu na mbinu tutakazojifunza katika maandalizi yetu ya mechi hiyo,” alisema Mayanja raia wa Uganda. 

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV