Na Saleh Ally
GUMZO sasa ni mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro, kwamba alionyesha kuibana Simba kwa makusudi na kuipendelea Yanga.
Mashabiki wengi wanajadili kila namna kuhusiana na suala hilo na huenda wachache sana wanaweza kuwazungumzia waamuzi wasaidizi Samuel Mpenzu wa Arusha na Ferdinand Chacha wa Mara, ambao waliboronga na kuchangia Saanya kufanya madudu.
Kawaida ya Watanzania, tunapenda kukwepa hoja kupitia visingizio visivyo na hoja za msingi. Lakini hili la Saanya nalo ni vema kulijadili, ingawa mimi ninapenda kupita njia tofauti kidogo.
Napenda kulijadili kuanzia Tambwe anapokea mpira akiwa na beki Novaty Lufunga, hadi anafunga na kwenda kushangilia.
Tambwe na bao:
Utaona pasi ya Mbuyu Twite ilivyoonyesha ubora, mpira mzuri wa ‘kuchop’ ambao uliinuka na kutua sehemu ya upande mmoja wa Tambwe ambaye anaacha upite kwa kugusa kifua kidogo kabla ya kufunga bao hilo.
Tambwe aliushika huo mpira, kwa kuusukuma kidogo mbele yake wakati akigeuka na baadaye akauwahi na kwenda kufunga.
Nianze na namna alivyogeuka, inaonyesha ukomavu na kwamba ni mshambuliaji mwenye njaa ya kufunga, safari hii akiwa anawafunga Simba bao la tatu katika mechi nne.
Kugeuka kwake, pamoja na makosa ya mkono kunaonyesha ubora wa lengo la kutaka kitendo sahihi katika muda mwafaka.
Lakini, kitu ambacho nilikiona ni bora kabisa na cha kiwango cha juu alichokionyesha Tambwe ni namna alivyofunga baada ya kutazamana uso kwa uso na kipa Vincent Angban.
Kipa huyu kwa sasa ndiye bora zaidi katika Ligi kuu Bara. Pamoja na juhudi zake za kujipanga vizuri kwenye lango, utulivu wa kutisha wa Tambwe ulimfanya asiwe na uwezo wa kuzuia lolote na kumpa nafasi ya kufunga bao safi utafikiri alikuwa anapiga mkwaju wa penalti.
Naweza kusema, ukiachana na kosa la kushika, umaliziaji wa Tambwe ulikuwa wa kiwango cha juu na bora kabisa.
Lufunga Vs Tambwe:
Kweli Tambwe amefunga bao kwa utulivu na ufundi wa juu kabisa. Lakini hali halisi inaonekana hata kama asingeshika, basi alikuwa na asilimia nyingine 75 ya kufunga bao hilo kutokana na kosa la ‘kitoto’ la beki Lufunga.
Unaweza kusema bado ni kinda, lakini kosa lake lilikuwa la ‘kitoto’ kabisa. Katika kuangalia kwangu mpira hata kama ingekuwa ni ndondo mtaani kwetu, pia ni aghalabu kuona beki anakaba akiwa nje ya lango lake.
Wakati Tambwe anageuka upande wa kulia kwake, Lufunga alikuwa nje, upande wa mkono wake wa kushoto. Sasa angeweza vipi kumzuia Tambwe asiende hata kama ameshika?
Kwani hata kama asingeshika, bado Tambwe alikuwa na nafasi ya kugeuka ndani na kwenda kufunga. Lufunga alikuwa mlinzi anayelinda benki lakini amelala kwenye uzio wa nyumba jirani.
Kawaida beki anatakiwa awe upande wa lango lake na si nje. Hakika alichofanya Lufunga ni kitu nadra kutokea kwa mabeki imara au walio makini na kazi zao. Anatakiwa kubadilika na ajifunze kwamba, pamoja na kulia Tambwe alishika, basi naye alikuwa sehemu ya tatizo hilo kwa asilimia kubwa sana.
Ndiyo maana naweza kusisitiza, kumlaumu Tambwe katika hili ni kupoteza muda. Yeye ni fowadi, anataka bao kwa njia zozote na itakavyowezekana.
Saanya na mkono:
Mwamuzi msaidizi Ferdinand Chacha aliyekuwa ‘line two’ unaweza usimlaumu hapa hata kidogo kwa kuwa Tambwe aligeuka ndani.
Akigeuka ndani, lazima atakuwa anampa mgongo, pia ni vigumu kwake kumuona kwa kuwa mkono ulioshika ulikuwa ndani. Pia Lufunga alikuwa upande wa nje, hivyo ilichangia kumzuia mwamuzi huyo msaidizi kuona kwa uhakika pia.
Lakini Saanya alikuwa ndani na hakuwa mbali na eneo la tukio, hata kidogo Saanya hawezi kuinua mdomo na kusema hakuona.
Kisheria, kama kuna kosa limetokea, mwamuzi msaidizi hakuliona, basi mwamuzi wa kati anaweza kumsaidia na ndiyo jambo ambalo Saanya alitakiwa kumsaidia.
Wakati mwamuzi msaidizi alikuwa anasita, Saanya alionyesha kati, huenda naye aliamini alikuwa amesaidiwa kwa usahihi maana hakuwa na uhakika. Ndiyo maana akatumia sekunde kadhaa kumuangalia mwamuzi wa kati ambaye ni kiongozi wake katika mchezo huo, alipoelekeza, naye akachukua maelekezo mara moja.
Tambwe na kushangilia:
Awali nilisema hauwezi kumlaumu Tambwe kwa kufunga baada ya kushinda, hilo naliwekea msisitizo. Lakini nimtupie lawama yeye na wachezaji wengine wa Yanga kwa kitendo chao cha kijinga cha kwenda kushangilia upande wa Simba ambao waliona wameonewa.
Hapa tutakuwa tunazungumzia weledi, kwani imekuwa ni kawaida kwa wachezaji kutaka kwenda kushangilia upande wa mashabiki wa upinzani.
Funga bao, nenda kwa mashabiki wako. Mara ngapi kwenye La Liga au Premier League unaona mchezaji anafunga halafu wakati anapokimbia anagundua kule anapokwenda si sehemu sahihi kwa kuwa si kwa mashabiki wake unaona anakata kona na kupita nyuma ya goli kwenda kwa mashabiki wake?
Kwani wachezaji wa hapa nyumbani huwa hawaoni au wakiangalia mpira wanaangalia kipi? Kwenda kwa Tambwe Simba wakiwa na jazba, wakaona njia nyepesi ni kumshambulia kwa viti.
Kwangu siungi mkono hata kidogo kwa mashabiki hao wa Simba ambao leo wamechangia timu yao kuondolewa kwenye Uwanja wa Taifa baada ya serikali kuchukizwa na upuuzi huo.
Kwani hawakuwa na njia nyingine, wakati mwingine wangeweza kupunguza hasira zao kwa maneno. Tunaona Ulaya, wanazomea kama sehemu ya adhabu. Hao waliovunja viti hawajui hata bei ya kiti kimoja!
Lakini Tambwe alikuwa sehemu ya chanzo cha kuwapandisha jazba zaidi na kuna haja ya kuwa na mabadiliko. Wachezaji waachane na mambo utafikiri yale ya kutaka kushindana na mashabiki wa upinzani na badala yake watumie muda mchache wa furaha zao, kushangilia na mashabiki wao.
Tambwe, Tambwe, bao safi Tambwe, Tambwe.What a waste!!
ReplyDeleteMi ni Simba ila ukweli ni kuwa pamoja na kuwa Tambwe alishika, Lufunga alikaba hovyo sana. Alitakiwa amuweke Tambwe mbele yake na kwa urefu wake angeokoa na kichwa. Bao safi la Ajib naona watu wengi wanalipotezea kwa kuwa halikuleta zogo
ReplyDeleteNimekuelewa kinoma salehe jembe umeelezea vizuri kweli kuliko huyu mwenzio shaffih anaetetea utumbo kabisa dadeki
ReplyDeleteKaka ushaanza kupoteza mwelekeo kwasababu haukutaka kueleza ukweli zaidi ya kuonesha ushabiki kwenye analysis yako
ReplyDeleteTuache kuzungumzia goli LA Tambwe aliye tumia mkono kusaidia mpira utoke katika mabeki na kufunga,tuzungumzie mechi nzima Kama goli LA Ajibu faulo Za Yondani,Ndio zilizopelekea wachezaji kupaniki na mashabiki pia,unaona ni jinsi gani waamuzi walikuja na matokeo yao.Nadhani Hata goli LA Ajibu lilikuwa bora na basi ilikuwa bora kwahiyo tuzungumzie mechi kwa jumla na Si kutetea mpira WA kihuni ambao utasababisha mechi ijayo kuwa ya kihuni zaidi timu zikiogopa kufanyiwa uhuni watajipanga kufanya uhuni nao.
ReplyDelete