October 26, 2016

ALI KIBA (KUSHOTO) NA DIAMOND


Na Saleh Ally
KAMA una simu inayoweza kufungua mitandao ya kijamii, basi ukizubaa utakuwa na bahati ya kushuhudia madudu tu na simu hiyo haitakuwa na faida kwako hata kidogo.

Mitandaoni kuna mambo mengi sana yanaendelea na hayana maana hata kidogo ingawa wanayoyaendeleza huamini wana uwezo mkubwa wa kuzungumza mambo na wanachosema ni sahihi hasa.

Kwenye Facebook, Instagram na Whatsapp ndiko jalala la kila asiye na uwezo kufikiri au kutafakari na kulichambua jambo. Ili mradi kuna uhuru wa kutoa maoni, basi kila mmoja ‘anatapika’ anachoona ni sawa. Hata vile vilivyojaa ujinga, viko mitandaoni na huko vina thamani kubwa kwa kuwa ndani ya mitandao hakuna kipimo cha madudu.

Nimejifunza mengi na ajabu zaidi, wachangiaji wa mambo mengi wasiojua mambo, hujirahishia njia ya uchangiajikwa kuporomosha matusi. 
Kutukana tu, ni sehemu ya kuonyesha uwezo mdogo wa upambanuzi wa hoja pia inathibitisha mchangiaji ubongo wake una njaa ya ufikiri kwa kiasi gani, lakini hauna uwezo wa kushiba kabla ya kuendelea na kazi yake.
Wiki iliyopita, wasanii Nasibu Abdul ’Diamond’ na Ali Saleh ‘Ali Kiba’ walikuwa ni kati ya wale waliopata nafasi ya ushiriki wa tuzo za MTV Mama ambazo zimefanyika nchini Afrika Kusini na wote walipata nafasi ya kutumbuiza. 

Diamond alitumbuiza na wacheza shoo wake, Kiba akatumbuiza akiwa na Sauti Soul wa Kenya ambao wamemshirikisha katika wimbo wao wa ‘Unconditionally Bae’.

Nianza kwa kuwapongeza Diamond, kwamba walifanya kazi nzuri kabisa. Mapungufu yalikuwepo kwa kila mmoja wao, kama Diamond na sauti kuonekana ni kama ni mtu anayepumua kwa nguvu lakini Kiba pia hakuwa na muda wa kutosha baada ya kuimba sehemu ya ubeti wake na kiitikio ambacho kilipunguzwa. Haikuwa rahisi kuweza kuona ubora wake vizuri lakini hakika, vijana hawa wa Kitanzania wanastahili pongezi.

Shoo ya Diamond, ilikuwa bora kuliko nyingine zote usiku huo ukumbini jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Lakini mitandaoni badala ya mjadala bora wa nani alifanya nini, kipi kilipungua na wapi kiongezwe, matusi ndiyo yametawala.

Mimi niliweka video za vipande vya shoo zao kwenye ukurasa wangu wa Instagram, lengo likiwa ni kuongeza kuwasambaza vijana hao wa Kitanzania ambao wanaendelea kuleta heshima na wanawapa changamoto wale ambao hawajafikia huko.

Diamond na Kiba si wasanii wa kwanza kuleta heshima nchini. Lakini hadi wamefikia hapo lazima kabla walifikiri kuwa kama fulani, mfano Lady Jayedee au AY na wengine ambao walikuwa wakifanya vema kimataifa.

Ajabu kabisa ni kwamba, walio mitandaoni wanajulikana kama Team Kiba na Team Diamond. Hawa ni watu ambao wako kwa ajili ya kusifia upande mmoja na kuupaka matope upande mwingine.

Team Kiba hakuna wanaloona ni zuri la Diamond, Team Diamond kazi yao ni kuponda tu upande wa Kiba. Kila unachofanya kama mwanadamu kinakuwa na faida zake, hasara zake pia.

Ukipima, utaona Team Diamond na Team Kiba wanafanya kazi ya kupoteza muda, mambo ya kijinga pia ni watu wasiotafakari kwa kuwa wamejivika kaniki na wanajaribu kuisafisha kwa ‘jiki’ ambalo si jambo sahihi.

Kaniki inakuwa jinsi ilivyo, kila unapoifua ni lazima ukumbuke rangi yake, maana huwezi kuibadili kwa kuifua. Si rahisi kuwaongezea au kuwapunguzia Diamond na Kiba kwa maneno makali au matusi mitandaoni. 

Kama Kiba na Diamond watakuwa wanazipa nguvu hizo timu, basi hata wao watakuwa hawajui wanalolifanya na hawafuatilii historia ya muziki kwamba wapambe kama hao Team Kiba na Team Diamond, huko nyuma walikuwa ni sehemu ya kufa kwa makundi mfano TKM Wanaume na East Coast. 

Mashabiki badala ya kuburudika, wanaishi na chuki, wanaamini kwenye kutukanana na kukataa kila kizuri cha wanayemuona ni mpinzani. Hakuna wanaofanikiwa kwa kukataa mazuri ya waliojitahidi.

Anayefanya vizuri, jifunze kwake. Pia matusi hayajawahi kuingia kwenye historia yoyote ya mafanikio, badala yake wanaofanya hivyo huonekana ni mwendawazimu.

Vizuri kuepuka kugeuza mitandao kuwa maficho ya wajinga na wanaoweza kusema lolote. Badala yake, kama kweli nyie ni timu kwa ajili ya kuwasaidia wasanii hao ambao wote ni Watanzania, basi muwe na mijadala bora yenye lengo ya kujenga, si kila anayetukana ndiyo anaonekana hakuna kama yeye.

Kumbukeni hata hawa Diamond na Kiba, siku moja watakwisha na wengine watapaa kwenye nafasi zao, hili halina mjadakla, hivyo mnaweza kuwasaidia kuendelea kubaki juu kwa muda mrefu kwa mawazo bora, kukubali kazi ya mwingine na kukosoa kwa mlengo wa uadui na chuki tu! Vipi unaweza kuwa shabiki wa burudani, halafu ukatumia muda wote kusambaza chuki wakati lengo namba moja la burudani ni kuburudisha!




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic