October 29, 2016Huku Yanga ikimrejesha Kocha Hans van Der Pluijm, Zesco yenyewe ikionekana kukata tamaa kumzuia kocha wao George Lwandamina kuondoka, imempa masharti mwalimu huyo kabla ya kumpa kibali cha kuondoka.

Lwandamina anahusishwa na mipango ya kujiunga na Yanga kuchukua mikoba ya Mholanzi, Pluijm ambaye hata hivyo amekataliwa kujiuzulu na klabu yake baada ya kuchukua uamuzi huo kutokana na ujio wa Mzambia huyo wikiendi iliyopita.

Chanzo makini cha habari kutoka Zesco, kimesema baada ya kuona hawawezi kumbakisha kocha huyo, wamempa masharti ya kuhakikisha anaiwezesha timu hiyo itetee ubingwa wake wa Ligi Kuu Zambia.

"Asilimia za Lwandamina kubaki Zesco ni ndogo sana, hivyo mara baada ya kuona suala hilo, viongozi sasa wameamua kumwambia kocha huyo afanye kila linalowezekana kuhakikisha klabu hiyo inatetea ubingwa wake wa ligi kuu ili wacheze Ligi ya Mabingwa Afrika.

"Wameamua hayo baada ya kuona kwamba Lwandamina amevutiwa zaidi na Yanga, hivyo ili wasipoteze vitu vyote wameamua kumalizana naye kwa namna hiyo," kilisema chanzo hicho.

Lwandamina aliyewahi kuinoa timu ya taifa ya Zambia 'Chipolopolo', kwa sasa amebakisha mkataba wa miezi mitatu na Zesco ambao utaisha Januari, mwakani.

Zesco inashika nafasi ya nne katika Ligi ya Zambia baada ya kucheza mechi 24 na ina pointi 50, imeshinda mechi 14, imetoka sare nane na imefungwa mara mbili. Kinara wa ligi hiyo ni Zanaco yenye pointi 65 katika mechi 28.

MECHI TANO ZA MWISHO ZESCO
Okt 12, 2016 ZESCO 2-1 Lusaka Dynamos             
Okt 18, 2016 Red Arrows 1-4 ZESCO        
Okt 22, 2016 Zanaco 0-0 ZESCO          
Okt 26, 2016 Nkwazi 1-0 ZESCO
Leo Green Buffaloes v ZESCO

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV