Mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Yanga, Mrundi Amissi Tambwe amewaomba wapenzi na mashabiki wa Simba kutomchukia na kumuona kama adui yao kwa sababu ya bao aliloifunga timu hiyo Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Tambwe aliifungia Yanga bao ambalo lilizua utata mkubwa baada ya kudaiwa kabla hajafunga aliunawa mpira.
Bao hilo ndilo lilizua balaa kubwa katika mchezo huo ambapo mara tu baada ya kufunga ziliibuka vurugu kubwa zilizosababisha mashabiki wa Simba kuvunja viti zaidi ya 1781, wakilipinga.
Hata hivyo baada ya kumalizika kwa mchezo huo mashabiki hao wa Simba waliendelea kulipinga bao hilo huku baadhi yao wakionekana kumchukia mshambuliaji huyo ambaye msimu uliopita aliibuka mfungaji bora.
Tambwe ambaye alijiunga na Yanga akitokea Simba, amewataka mashabiki hao kutomchukia na kumuona kama adui yao namba moja kwa sababu ya bao lake hilo.
Alisema yeye kazi yake ni kufunga haijalishi kafunga kwa njia gani hivyo amewataka mashabiki hao wa Simba kulijua hilo kisha waendelee kumuona kama ndugu yao.
“Binafsi sina uadui na Simba hata kidogo, ila nasikitika kuona baadhi yao wananichukia na kuniona kama adui yao kwa sababu ya bao langu, hakika hiyo siyo sawa.
“Katika mchezo wa soka kazi ya striaka ni kufunga na haijalishi amefunga kwa staili gani kama niliwaudhi naomba wanisamehe, ila nawataka wajue kuwa kufunga ndiyo kazi yangu ambayo na nitaendelea kufunga kwa staili yoyote ile ili kuhakikisha naisaidia timu yangu kumaliza ligi kuu ikiwa katika nafasi nzuri na ikiwezekana kutwaa ubingwa,” alisema Tambwe.
soka
ReplyDelete