October 5, 2016Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, ameweka bayana kwamba lengo lake alilojiwekea la kutopoteza mchezo katika viwanja vya Dar limetimia ambapo sasa anaenda kupeleka moto huo katika mechi za mkoani, ambapo wanatarajia kwenda Mbeya kucheza na timu za mkoa huo.

Omog ameiongoza Simba kuchota pointi 17 katika mechi saba za timu hiyo za Dar, baada ya kushinda tano na sare mbili bila ya kupoteza hata mchezo mmoja ambapo sasa wanatoka nje ya Dar kwa mara ya kwanza tangu walipoanza kucheza mechi zao.

Kocha huyo ambaye amewahi kuinoa Azam, amesema anatambua ugumu unaopatikana katika kutwaa pointi za mkoani kutokana na timu nyingi kukamia pamoja na ubovu wa viwanja, lakini hilo kwake hatalijali kwa sababu anahitaji ushindi ambao utaendelea kukiweka kikosi hicho kileleni mwa msimamo.

“Lengo langu la hapa Dar limetimia tayari kwani hatujapoteza mchezo hata mmoja na sasa tunataka kuendeleza rekodi hiyo ya kutofungwa katika michezo ya mikoani licha ya changamoto ambazo zinapatikana katika viwanja vingi, lakini tutapambana.

“Moto huu tulioanza nao tunataka uendelee na hilo linawezakana kwa sababu tuna kikosi kinachoweza kuibuka na ushindi katika mazingira yoyote yale, pia morali yetu inaongezwa kwa sababu tunataka kuchukua ubingwa kwa msimu huu na hilo halitaweza kutimia kama tutashindwa kupata pointi katika michezo hiyo,” alisema Omog.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV