October 18, 2016

AZAM FC
Wakati leo Jumanne Oktoba 18, 2016 timu ya JKT Ruvu ya Pwani na Kagera Sugar zinafungua rasmi mzunguko wa 11 wa Ligi Kuu ya Mpira wa Miguu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), michezo mingine sita itafanyika kesho Jumatano Oktoba 19, mwaka huu wakati keshokutwa Alhamisi Oktoba 20, kutakuwa na mchezo mmoja tu.

Mchezo wa leo Na. 86 wa VPL utafanyika Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani kabla ya kesho Oktoba 19, mwaka huu kuendelea kwa mechi sita pia za mzunguko 11 wa kukamilisha raundi ya kwanza kwa msimu 2016/17.

Vodacom – Kampuni ya simu za mkononi inayoongoza nchini kwa kutoa huduma za kisasa za mawasiliano ndiyo mdhamini mkuu ligi hiyo ikisaidiana kwa karibu sana Kampuni ya kisasa ya vyombo vya habari yenye kurusha vipindi vyake kwa weledi na ubora wa hali ya juu ya Azam Televisheni (Azam Tv) na DTB- Benki ya kuaminika nchini kwa usalama wa fedha zako.

Kampuni hizo zinazong’arisha VPL, kesho zitakuwa sambamba kwenye kuchagiza michezo ya Ruvu Shooting ya Pwani ambayo itaikaribisha Mwadui ya Shinyanga kwenye Uwanja wa Mabatini uliuoko Mlandizi mkoani Pwani katika mchezo Na. 81 wa VPL utakaoanza saa 10.00 jioni.

Mchezo Na. 82 utakaozikutanisha Azam FC ya Dar es Salaam na Mtibwa Sugar ya Morogoro utafanyika saa 1.00 usiku (19h00). Mchezo huo utafanyika Uwanja wa Azam ulioko Chamazi – maskani ya Azam yalioko nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam wakati mchezo Na. 83 utazikutanisha timu za Ndanda FC na Mbeya City ya Mbeya kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Mchezo Na. 85 utazikutanisha timu za Tanzania Prisons ya Mbeya na Stand United itakayokuwa mgeni kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya huku mechi Na. 87 itazikutanisha Toto African ya Mwanza itakayocheza na Young Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati African Lyon itakuwa mwenyeji wa Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam kwenye mchezo Na. 88.

Ligi hiyo itaendelea tena keshokutwa Alhamisi Oktoba 20, kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ambako vinara wa ligi hiyo kwenye msimamo hadi sasa, Simba itakuwa mwenyeji wa Mbao FC ya Mwanza katika mchezo Na. 84.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic