October 8, 2016Yanga imecheza mechi sita na sasa ipo nafasi ya tano katika Ligi Kuu Bara lakini kocha wa timu hiyo, Hans van Der Pluijm amesema hiyo haiwezi kuwa sababu ya kuitoa timu yake katika mbio za ubingwa.

Pluijm raia wa Uholanzi ameipa Yanga mataji mawili ya ubingwa huo amesema kuwa, licha ya timu yake kusuasua atahakikisha wanatetea ubingwa wao.

Yanga ina pointi 11 katika nafasi ya tano, ikiwa imezidiwa na Simba inayoongoza ligi ikiwa na pointi 17. Hata hivyo Wanajangwani wamecheza mechi sita wakati Simba wamecheza saba.

Pluijm ambaye ni kipa wa zamani wa timu ya Taifa ya Uholanzi, amekiri ushindani kuongezekana maradufu katika ligi na timu nyingi zimeonekana kuikamia Yanga tofauti na wengine.

“Jamani! Tumecheza mechi ngapi na tumebakiza mechi ngapi? Sisi tumecheza mechi sita tu, iweje tuonekane hatuna nafasi ya kutetea ubingwa wetu? Hii si sawa kwani tuna mechi nyingi mbele yetu.

 “Kila timu inayokutana na Yanga inaonekana kucheza zaidi ya uwezo wake, lakini na sisi tunapambana kuhakikisha tunavuna pointi tatu muhimu. Bado ni mapema na tunaweza kutetea ubingwa,” alisema Pluijm ambaye amewahi kuzinoa Klabu za Berekum Chelsea na Medeama zote za Ghana.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV