Bao la kusawazisha la dakika 87 lililofungwa na Shiza Kichuya dhidi ya Yanga wikiendi iliyopita, wachezaji na mashabiki wa Simba walilifurahia, lakini kwa upande wa wapinzani wao lilivuruga mipango ya timu hiyo ya kulitetea taji lao la Ligi Kuu Bara.
Kichuya, alifunga bao wakati timu yake ipo nyuma kwa bao 1-0 hadi dakika hiyo baada ya kupiga kona iliyozama moja kwa moja wavuni baada ya kumshinda kipa Ali Mustapha ‘Barthez’ na kufanya mechi hiyo kuisha kwa sare ya bao 1-1.
Sare hiyo iliiwezesha Simba kuendelea kukaa kileleni kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 17 huku Yanga wakiwa na 11 katika nafasi ya tano.
Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, alisema matokeo hayo ya sare na Simba yameshusha morali ya wachezaji wake ambayo awali ilikuwa juu.
Pluijm alisema walikuwa wakihitaji pointi tatu ili kuipunguza kasi Simba ambayo haijapoteza hata mechi moja katika mechi saba ilizocheza.
“Nikiri sare na Simba, ilishusha morali ya wachezaji wangu.
“Kwani kwenye mechi hiyo, tulihitaji ushindi ili tupunguze kasi ya Simba.
“Baada ya matokeo hayo, wachezaji walikata tamaa ya kutetea ubingwa, lakini kama kocha nimejaribu kuwatengeneza kisaikolojia ili kurejesha morali yao iliyopotea na sasa wapo sawa,” alisema Pluijm.
0 COMMENTS:
Post a Comment