TWITE (KUSHOTO) |
Na Saleh Ally
NAJUA umewahi kusikia namna ambavyo mchezaji Mwinyi Kazimoto alivyolaumiwa, kwamba kuna mechi fulani au ile kwamba hakuonyesha kiwango kizuri katika mechi fulani na kusababisha timu yake kuyumba.
Hivi karibuni kumekuwa na taarifa za Kazimoto kushindwa kucheza vizuri katika mechi na badala yake kuonyesha kiwango bora mazoezini tu. Anapofikia kwenye mechi, anakuwa hana lolote.
Mijadala kama hii inakuwa si rasmi, lakini inaweza kuwahusisha hata baadhi ya watu wa karibu na Simba kwa kuwa hawaridhiki na mwenendo wa mkongwe huyo.
Kwa upande wa Yanga, Mbuyu Twite naye amekuwa akikosolewa kwamba kasi imepungua, huenda sasa hana msaada mkubwa sana na kikosi cha Yanga na wakati fulani ilifikia wako wakathubutu kusema, Yanga ilikosea kumuongezea mkataba.
Katika mechi ya Oktoba Mosi ambayo Yanga na Simba zilimaliza kwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kuna mengi yamekuwa yakijadiliwa.
Mfano Amissi Tambwe alinawa kabla, mwamuzi msaidizi alikataa bao la Ajibu na kadhalika. Lakini si rahisi kusikia anayesifia au kuelezea kazi nzuri kabisa iliyofanywa na wachezaji hao wawili.
Kazimoto, Mtanzania aliyekulia kisoka mkoani Mwanza na Twite Mkongomani mwenye uraia wa Rwanda, walifanya kazi hasa katika vikosi vyao.
Kocha wa Simba, Joseph Omog alimpanga Kazimoto namba kumi na moja. Kitu ambacho hakuna ambaye angeamini kama inawezekana kwa kuwa ni kawaida kumuona Kazimoto akicheza namba nane, sita na aghalabu namba 10.
KAZIMOTO (KULIA) |
Siku hiyo aliitendea haki namba hiyo na huenda ndiye mchezaji wa Simba aliyekuwa hatari zaidi kwenye ngome ya Yanga. Hili linathibitishwa na ilivyokuwa, mfano katika pasi na hata faulo alizochezwa.
Faulo 25 walizofanya Yanga ambazo zilikuwa nyingi zaidi ya Simba. Kazimoto aliangushwa mara tisa. Utaona alitibiwa uwanjani mara mbili na ndiye alikuwa dereva wa Simba kutokea kushoto pembeni mwa uwanja.
Baada ya Jonas Mkude kulambwa kadi nyekundu, Mzamiru Yassin ambaye uchezaji wake unaonekana anakuwa bora zaidi akicheza dimba la chini, akashuka namba sita ambayo aliitendea haki.
Kazimoto akavunja wingi ya kushoto, halafu akaendelea kukipiga sasa akiwa namba nane. Hakuna anayeweza kukataa kwamba Simba walionekana utafikiri wako sawa na Yanga kwa idadi na si pungufu.
Angalia, Juma Abdul ambaye ni hatari kwa krosi alipiga ngapi siku hiyo wakati akikabana na Kazimoto. Alimmaliza na kumtoa katika makali yake. Hata baada ya kurejea namba nane, bado aliendelea kuziba upande wa juu akicheza muda mwingi na mpira, “chukua nipe, chukua nipe”.
Kwa upande wa Yanga, mfumo waliokwenda nao ni ule wa ‘hub’ kama zilivyo timu za Waingereza. Hub ni sehemu ambapo kitu kinaweza kugeuka. Twite ndiye alikuwa akifanya kazi hiyo.
Ukiangalia vizuri mechi hiyo, Twite aligeuza mpira zaidi ya mara 12, yaani kuutoa kwenye matatizo na kuupeleka sehemu salama ili Yanga iendelee kuwa kwenye ‘play’.
Pasi ya bao la Tambwe lililozua utata, pasi murua ilitoka kwake. Kama Tambwe asingeshika na kufunga. Hakika gumzo pia lingekuwa ni pasi hiyo.
Mjadala wa alishika au hakushika, umeifunika pasi hiyo. Pia mijadala hiyo imefunika alichokifanya Twite ambaye ndiye aliwafanya Vincent Bossou na Kelvin Yondani kucheza wakiwa hawana presha.
Hans van der Pluijm alimtumia kama ule mfumo wa Man City ya msimu uliopita. Bossou au Yondani wakirudishiwa mipira, basi lazima wamkabidhi yeye. Kama amebanwa ndiyo watahamisha mbele au mbali.
Twite alipiga pasi nyingi zilizofika, huenda kuliko mchezaji yeyote wa Yanga. Utulivu katika daraja alilojenga uliifanya Yanga kutulia zaidi nyuma.
Hata kipindi Yanga imezidiwa na Simba, utaona ni baada ya Twite kuingia hasa kutokana na mabadiliko ya Simba ambayo waliwaingiza vijana zaidi kama akina Mohamed Ibrahim na yeye akiwa ameishatumika sana.
Katika mechi hiyo ya watani, hakika wakongwe hao wawili, Kazimoto na Twite walionyesha wanaijua kazi yao na kama wakiendelea na kiwango hicho, basi watamaliza msimu na mafanikio makubwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment