Kuna ule msemo hivi, "Ukimwaga ugali wenzio wanamwaga mboga! Sasa Simba imepanga kumwaga mboga baada ya kuona nahodha wake, Jonas Mkude, kamwaga ugali.
Simba inaona Mkude anadengua kusaini mkataba mpya wao watamsajili kiungo mwenye uwezo zaidi yake.
Achana na hiyo, Simba pia imepanga kumpiga benchi Mkude katika michezo yao inayokuja ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara, kwani haijapendezwa na kitendo cha nahodha huyo kusema yupo tayari kusaini hata Yanga kama atazinguliwa na timu yake hiyo.
Tayari Mkude amevuka mtego wa kwanza aliowekewa na Simba kwamba kama asingetokea mazoezini angekatwa mshahara wake lakini kiungo huyo ameenda mara moja katika mazoezi hayo ambapo jana ilikuwa siku ya nne ya mazoezi hayo kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa mabosi wa Kamati ya Usajili ya Simba, amesema: “Tunataka kumsajili kiungo mkabaji mwingine katika usajili huu, haya mambo ya Mkude hayajatupendeza.”
“Inaonekana Mkude anatudengulia kuongeza mkataba mwingine wa miaka miwili kutoka ule wa sasa ambao unaisha Januari mwakani, awali tulipanga kuongeza beki wa kati, beki wa kulia na kipa pekee.
“Lakini baada ya Mkude kutudengulia kusaini mkataba, tumeona ni bora tukamsajili kiungo mwingine mwenye uwezo kama wake, hatutaki tuwe na mchezaji mmoja tegemeo kwenye timu,” alisema bosi huyo.
Zacharia Hans Poppe ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, akizungumzia hatua hiyo, alisema: “Tunaendelea kufanyia kazi ripoti tuliyokabidhiwa na kocha wetu, hayo mengine tutaangalia baadaye.”
Awali, Mkude amesema kuwa, hajawahi kuzungumza na viongozi wake kuhusu mkataba mpya na anashangaa kuhusu kuelezwa kwamba hapatikani hewani.
Kuhusu kuwazimia simu viongozi wa Simba, Mkude alisema: “Ndiyo nilizima simu kwani wao walisema mimi nimeshasaini mkataba mpya wakati si kweli, hivyo nikawa napata usumbufu kwa ndugu wengine wakitaka kujua sababu za mimi kufanya hivyo bila kuwashirikisha na wengine waliniomba fedha wakati si kweli. Haikuwa haki.”
Usajili wa dirisha dogo unaoendelea sasa, ulianza Novemba 15, mwaka huu na unaisha Desemba 15.
0 COMMENTS:
Post a Comment