December 13, 2016






Na Saleh Ally
MIAKA 14 sasa, mashabiki wa Arsenal wamekuwa wakitamani kuiona klabu yao kwa mara nyingine ikibeba ubingwa wa England ambao imewahi kuuchukua mara 13.


Mashabiki hawataki rekodi tena, badala yake wanachotaka ni kuona sasa wakibeba ubingwa huo ambao umegeuka fimbo kwao, mashabiki wa Man United, Chelsea na wengine wamekuwa wakiwatupia maneno ya kejeli kuhusiana na ubingwa huo. 

Liverpool, hawawezi kuinua mdomo hata kidogo na kuwabeza Arsenal maana wao, mara ya mwisho waliuchukua ubingwa huo msimu wa 1989/90.

Wakati kila shabiki wa Arsenal akionekana kuchoshwa na hilo, mhanga wa jambo hilo ni Kocha Arsene Wenger raia wa Ufaransa ambaye alijiunga na Arsenal mwaka 1996 akitokea Japan alipokuwa akiinoa Grampus Eight ya Nagoya.



Hauwezi kusema hana mafanikio, hadi sasa kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya ndiyo hajaliweka nguvuni na inaonekana ukiachana na fainali, hana mafanikio makubwa upande wa michuano iliyo chini ya Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa).

Kikubwa ambacho Wenger amekuwa akijisifia ni kuifikisha Arsenal kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya karibu kila msimu bila ya kujali ameshika nafasi ya pili au ya nne kwenye Ligi Kuu England. Kwa viongozi, yanaweza kuwa mafanikio makubwa sana kwa kuwa kushiriki michuano hiyo, ni biashara nyingine kubwa kwa kuwa hesabu ya klabu, kwanza ni kuingiza faida.

Ukiangalia kwa miaka 20 rekodi zinaonyesha Arsenal imeendelea kubaki na Wenger kwa muda wote na imefanikiwa kubeba makombe tofauti 12 na Ngao za Jamii tano ikiwa chini yake.


Bado kuna timu zimebadili makocha rundo, mfano Real Madrid ndiyo wanaonekana hawataki mchezo na si wavumilivu kuliko timu nyingine yoyote duniani kwa kuwa wamefanikiwa kubadili makocha 21 wakifuatiwa na Chelsea ambao wamebadili makocha 16.

FC Barcelona, timu nyingine yenye mafanikio zaidi duniani, yenyewe ndani ya miaka 20, imebadili makocha 13, Bayern Munich ambao ni vigogo wengine wa soka duniani, wamebadili mara 12 huku Liverpool wakifuatia kwa kubadili makocha wanane na Man United wamebadili makocha wanne tu.

Utaona, katika timu hizo ambazo zimekuwa zikichukua vikombe mfululizo, Man United pekee ndiyo imebadili makocha wachache ndani ya miaka 20. Tena inaonekana United ndiyo wamebadili makocha wengi haraka zaidi hasa baada ya kuondoka kwa Alex Ferguson ambaye alidumu kwa zaidi ya miaka 28.


Liverpool, wao pekee ndiyo wanaweza kuwa mfano mbaya, kwamba pamoja na kubadili makocha mfululizo hadi kufikia wanane, bado hawajafanya makubwa na wamebaki kuonekana kuwa Liverpool ya enzi hizo ndiyo ilikuwa moto hasa unapozungumzia makombe, si hii ya sasa.

Timu nyingine zilizobaki, Madrid, Barcelona, Bayern na hata Chelsea, zinamchongea Wenger kila kukicha kwamba kama kocha hajachukua makombe, hasa sababu ya kubaki.

Arsenal wanaendelea kupishana kati ya mashabiki na uongozi ambao unaona uwepo wa Wenger ni kuingiza faida na hakuna presha kubwa. Hasa mifano ya uongozi inaonekana ni kuondoka kwa Ferguson na namna Man United ilivyoyumba.


Inawezekana huu ni msimu wa mwisho wa Wenger kuamua kwamba anastahili kubaki au la! Tena akiwa ameonekana kuimarika zaidi ukilinganisha na msimu uliopita.

Kama utachukua msimamo wa Ligi Kuu England katika raundi ya 15, inaonyesha msimu 2016-17 kumekuwa na mabadiliko ya mafanikio kuliko ule uliopita wa 2015-16.

Msimu wa 2015-16, baada ya Arsenal kucheza mechi ya 15, ilikuwa ikionyesha ina pointi 30 katika nafasi ya pili nyuma ya Leicester ambao walikuja kuwa mabingwa mwisho wa ligi hiyo.

Msimu huu, hadi jana walikuwa kileleni na hata kama wangeshushwa baada ya mechi ya Chelsea, lakini wana pointi 34, mbili zaidi ya zile za msimu uliopita.


Tena unaona msimu huu, Arsenal ndani ya mechi 15, wameshinda 10, msimu uliopita walishinda tisa. Wana sare nne, msimu uliopita walikuwa na tano, wamepoteza moja, msimu uliopita walikuwa wamepoteza tatu.

Kuna jambo Wenger anaweza kufanya jambo kama ataendelea kushikilia mwendo huo na kuuongezea kasi. Akashindwa, basi litakuwa chaguo lake na huenda presha ikapaa na kuwazidi viongozi na mwisho, akafungashiwa virago.

MSIMU WA 2016-17
Timu GP    W    D   L GD PTS
1. Arsenal 15   10    4   1 21 34
2. Chelsea 14   11    1   2 21 34
3. Liverpool         14     9    3   2 17 30
4. Man City         15     9    3   3 13 30
5. Tottenham         14    7    6   1 14 27

MSIMU WA 2015-16
             GP        W    D         L          GD       Pts
1. Leicester       15    9        5          1          11       32
2. Arsenal          15     9        3          3          14       30
3. Man City    15   9    2          4          14       29
4. Man United  15  8    5          2          10       29
5. Tottenham   15   6   8          1          13       26



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic