January 11, 2017Kocha Mkuu wa timu ya Mshikamano ya Dar es Salaam inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Hamisi Kinonda amefunguka kuwa ilibaki kidogo wachezaji wake wafie uwanjani katika mchezo wao wa juzi dhidi ya Lipuli ya Iringa kutokana na kichapo kikali walichokumbana nacho.

Katika mchezo huo wa Kundi A ambao Mshikamano ilikubali kichapo cha mabao 2-1 katika Uwanja wa Kichangani, Iringa,inadaiwa kuwa wachezaji wa Mshikamano walipigwa na askari waliokuwa wakilinda amani uwanjani hapo baada ya kumzonga mwamuzi.

Akizungumza kocha huyo alisema chanzo cha wao kukumbana na kipigo hicho ni baada ya mwamuzi wa pembeni kumshambulia mchezaji wao, Muhsin ambapo katika kujihami ndipo wachezaji wake wakaanza kupigwa virungu na askari waliokuwa uwanjani hapo.

“Yaani tumekutana na wakati mgumu sana Iringa kwa tukio zima lilivyotutokea, kule wenyewe wana msemo unasema kwamba mgeni lazima aache pointi tatu kivyovyote vile na viongozi wote wanakuwa nyuma ya timu mwenyeji na kuisapoti ili ipate kushinda.

“Sisi ndiyo tulikuwa wa kwanza kupata bao na likadumu hadi kipindi cha kwanza kinakwisha, wao wakaja kusawazisha. Zilipomalizika dakika tisini, zikaongezwa sita.

“Dakika ya mwisho kabisa mwamuzi akatoa maamuzi ya utata baada ya kuwapa penalti wenyeji ambayo haikuwa halali maana ulikuwa mpira wa kona mabeki wangu wakaokoa lakini refa akaweka penalti ambapo wachezaji wangu wakahamaki na kuanza kumzonga.

“Lakini ghafla akatokea mwamuzi wa pembeni ambaye akaenda kumpiga mchezaji wangu kichwa, sasa katika hali ya yeye kujihami ndipo askari na watu wa usalama waliokuwa uwanjani wakaanza kuwapiga kwa virungu wachezaji wangu na timu nzima bila ya kuangalia sehemu gani ambayo wanapiga.

“Kutokana na tukio hilo vijana wakataka kutoka uwanjani na kususia mechi lakini kwa sababu hatukutaka kushushwa daraja kutokana na kugomea mchezo nikawaamuru warudi uwanjani tumalizie mchezo.

“Niweke wazi kwamba tumeumizwa na hali hiyo tuliyokutana nayo Iringa na sisi kuepuka maafa zaidi baada ya mechi tu tulichukua gari na kurejea Dar kwani tuliamini kama tukilala pale kungekuwa na hatari ya wenyeji wetu kuja kutufanyia unyama zaidi ya ule wa uwanjani.


“Ukiacha kupigwa virungu na pia wachezaji wa Lipuli walikuwa wanawapiga ngumi za waziwazi wachezaji wangu na utaona kuna mmoja ambaye alivimba jicho baada ya kupigwa huko lakini mwamuzi wala hakuchukua maamuzi yoyote yale,” alisema Kinonda. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV