January 8, 2017Mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva amesema wamekikubali kipigo kutoka Azam FC lakini bado wana nafasi ya kujirekebisha.

Yanga imepokea kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Azam FC katika mechi ya mwisho ya Kundi B katika michuano ya Mapinduzi. Mechi hiyo imechezwa jana kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Msuva amesema mashabiki wasikate tamaa, waendelee kuwaunga mkono nao kupitia benchi la ufundi na wao wenyewe watajirekebisha.

"Mpira una matokeo matatu, kushinda, sare au kufungwa. Kufungwa imetutokea sisi, lakini hatuna ujanja. Nawaomba mashabiki wasikate tamaa na badala yake waendelee kutuunga mkono.

"Benchi la ufundi wameona makosa yetu, sisi wachezaji tumeona na tutayafanyia kazi na kuendelea kufanya vizuri.

"Unajua kikubwa ambacho ni kizuri tumevuka kwenda nusu fainali hivyo tuna nafasi ya kujirekebisha kwenye nusu fainali na ikiwezekana fainali," alisema.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV