January 9, 2017

Na Saleh Ally
MWAKA 2003, SC Villa ilibeba ubingwa wa Afrika Mashariki baada ya kuitwanga Simba ya Tanzania bao 1-0, katika mechi ya fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mandela jijini Kampala, Uganda.

Shujaa alikuwa ni Mkenya, Vicent Tendwa ambaye alifunga bao hilo pekee. Lakini gumzo na nyota wa mchezo huo alikuwa ni Mtanzania, Shaaban Kisiga ambaye ndiye alitoa pasi iliyozaa bao hilo la ushindi.

Kisiga alikuwa mmoja wa wachezaji tegemeo wa SC Villa na alianza kuuonyesha umuhimu wake tangu mwanzo wa michuano hiyo ambayo Simba iliishi kimkandamkanda ikitawaliwa na ukata hadi kufikia wakati fulani kuazima jezi.

Baadaye Simba ilimrejesha Kisiga nyumbani baada ya kuona vitu vyake. Maana yake hakuwa na nafasi ya kuendelea zaidi kucheza nje, sasa bado anaitumikia Ruvu Shooting ya mkoani Pwani.

Ukipiga hesabu ya wachezaji wa Tanzania waliocheza Uganda na wa kwao waliocheza hapa, kuna tofauti kubwa. Wao wamekuwa wakija kwa wingi na wengi wamechota mamilioni ya fedha na mfano mzuri ni Emmanuel Okwi ambaye leo kila siku analiliwa arejee Tanzania.

Tanzania na Uganda, nchi yetu ni kubwa zaidi, utajiri kifedha ni juu zaidi na hasa unapozungumzia uwekezaji, mfano wadhamini au watu waliotayari kusajili kuzisaidia timu. Ndiyo maana Waganda wengi wanakimbilia hapa wakitaka kucheza.

Watanzania wanasema hawawezi kwenda kucheza Uganda kwa kuwa timu zao zinalipa kiwango cha chini sana! Ajabu hata hawa wanaozisaidia timu za Tanzania inaonekana kuwa hawana msaada endelevu badala yake ni ushindi wa muda.

Simba na Yanga ni mfano mzuri, hazijawekeza kwa vijana ambao baadaye wangeisaidia Tanzania kuwa na wachezaji wengi wanaokwenda nje ya Tanzania na siku nyingi Tanzania ikawa bora na kujijenga Afrika.

Wengi wanataka zishinde leo pekee, Uganda inaendelea kuzalisha vipaji na uongozi wenye lengo la kufanikisha lengo fulani. Hapa viongozi wengi ni wale wanaotaka kujinufaisha wao na rafiki zao au watu wa kabila moja au waliotoka nao kijiji kimoja.

Uganda imerejea na kufuzu katika Kombe la Mataifa Afrika. Mara ya mwisho walifuzu mwaka 1978, safari hii wamefuzu tena na juzi Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kupitia tuzo zao wameitangaza Uganda kuwa timu bora ya Afrika.

Kutoka Uganda na Tanzania si mbali, ukiumaliza Mkoa wa Kagera upande wa Kaskazini, unakuwa umeingia kwenye ardhi iliyotoa timu bora ya taifa Afrika. Lakini Magharibi ya Tanzania kuna DR Congo wao kushiriki Kombe la Mataifa Afrika si jambo geni hata kidogo na halina ugumu wowote.

Tanzania bado ipo inaendelea kusuasua. Kisingizo kilikuwa ni Afrika Mashariki kumezubaa na hakuna anayefanya vizuri, leo Uganda inakwenda Afcon ikiwa timu bora ya taifa. 

Kenya ina wachezaji wanaocheza Premier League ya England, League 1 ya Ufaransa, waliowahi kucheza Serie A ya Italia, bado kwenye riadha ndiyo usiseme. Sijui tuna kisingizio gani kingine.

Baada ya Kisiga kufanya vizuri Uganda, vipi hakuendelea au hakutokea mwingine. Kawaida viongozi wakisikia Mtanzania anafanya vizuri, wanakimbilia kumvuta na kumrejesha nyumbani, mwishowe ‘wanampoteza’.

Kocha SredojevicMilutin ‘Micho’, alifanya kazi hapa, akaonekana hana kitu lakini leo ndiye kocha wa timu bora ya taifa Afrika. Micho ndiye mwenye mchango mkubwa kwa kuwa anawauza wachezaji wengi wa Uganda nje ya Afrika na hasa Ulaya Mashariki. Leo wachezaji hao wamegeuka na kuwa msaada mkubwa Uganda.

Tukubali, siasa za Simba na Yanga tulizozikumbatia zinatumaliza. Tukubali, viongozi tulionao katika vyama na TFF ni sumu kuu ambayo itatubakiza hapa milele kwa kuwa lengo lao ni kujiendeleza wao na si mpira wa Tanzania.

Tubadilike, tukatae ujinga. Tusiwe bendera fuata upepo, tusishawishiwe na vishilingi vya maji ya kunywa. Kama hatutaki, basi tusubiri kuishangilia Uganda katika Afcon na baadaye tutahamia Kenya, Rwanda, Burundi kwa kisingizo ni jirani zetu!

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV