February 10, 2017


Na Saleh Ally
JANUARI 31, 2015, kiungo kinda raia wa Nigeria, Onyinye Wilfred Ndidi, alianza kuichezea KRC Genk ya Ubelgiji ambayo alijiunga nayo akitokea katika moja ya akademi ya Nath Boys ya kwao nchini Nigeria.

Desemba 3, 2016, alijiunga na mabingwa watetezi wa England, Leicester City na Januari 14, 2017 alicheza mechi yake ya Ligi Kuu England dhidi ya vinara wa ligi hiyo Chelsea na timu yake ikashushiwa kipigo cha mabao 4-0.

Januari 2015 unamzungumzia Ndidi anayecheza katika kikosi ambacho sasa tayari ni saizi ya Mtanzania Mbwana Samatta. Mwaka mmoja baadaye, Ndidi ni mtu mwingine kabisa, yuko katika kikosi cha Leicester, mabingwa wa England na kama utaweka vizuri ni kwamba alikuwa anachuana na wachezaji kama akina Eden Hazard au siku nyingine watu kama Zlatan Ibrahimovic au Mesut Ozil.


Sitaki kuzungumzia sana suala la umri kwa kuwa Ndidi ana miaka 20 tu hadi sasa na Wanigeria au watu wa Magharibi wamekuwa wakijaribu mara kwa mara kushusha. Lakini hoja ya msingi ni mafanikio au hatua za kiungo huyo.

Kama Ndidi yuko Leicester kwani kipi kitakachomzuia Samatta kufika hapo? Huenda nahodha huyo wa Taifa Stars ambaye wote tunamjua ni mtu mwenye malengo na anayejituma kweli atakuwa amepata changamoto kuu.

Maana ndani ya miezi minne, tayari wachezaji wawili ambao anacheza nao mmoja amekwenda Bundesliga na mwingine kapiga hatua hadi Premier League. Kama unakumbuka, Mjamaica Leon Bailey amejiunga na Bayer Leverkusen ya Ujerumani. Huyu pia alikuwa akicheza na Samatta katika ushambulizi na wakati mwingine waliunda pacha bora kabisa.

Hizo ni kati ya ligi tatu bora za Ulaya na duniani kote. Maana yake wana nafasi ya kusonga mbele zaidi na hii inathibitisha jambo moja jingine kwamba Samatta hakukusea kwenda Ubelgiji kwa kuwa ni njia sahihi.

Wengi wangependa kuona anakwenda nchi kama Ufaransa na huo ndiyo ulikuwa mjadala wakati yeye anaondoka kwenda nchini Ubelgiji baada ya kuiacha TP Mazembe.

Kwa hiyo hesabu zake zilikuwa sahihi na alistahili kwenda kujiunga na timu ya Ubelgiji akiamini akifanya vema ana nafasi ya kwenda katika moja ya ligi kubwa. Wako wanaotoka kutoka alipo kwenda katika ligi hiyo.

Maana yake kwa yeye, mfano umfananishe na Ndidi au Bailey, utaona Samatta amecheza michuano mikubwa kama ile ya Kombe la Dunia akiwa na TP Mazembe, tena dhidi ya timu kubwa kama Inter Milan na kadhalika.

Hivyo hali ya kujiamini na uwezo alionao haina shida wala shaka kwamba ana uwezo wa kufika huko walikofikia wenzake.

Lakini kitu kimoja, Bailey na Ndidi ni kama wamempa ujumbe kwamba safari yake kwenda nje ya Ubelgiji haihitaji kusubiri muda mrefu sana.


Badala yake juhudi za dhati kutaka kuondoka zinaweza kubadili mambo muda wowote na yeye akaanza safari hiyo mapema.

Ukweli ni hivi; Samatta yuko Ubelgiji akiwa njiani kwenda Ufaransa, Italia, Ujerumani, Hispania au England na lazima aende kama anataka kuwa kati ya wachezaji walioandika mafanikio makubwa katika soka.

Hivyo hana sababu ya kusubiri sana kwa sababu nyingi kwamba anahitaji kuzoea angalau misimu miwili, mitatu au zaidi. Badala yake ni kuangalia njia sahihi ya kuondoka na kufikia anapotaka.

Bailey na Ndidi ni kama wamefunga kamba za viatu vyake na kumueleza kwamba asichoke na anaweza kuzifungua baada ya kutua katika moja ya ligi hizo bora duniani. Mimi naamini inawezekana na Samatta namuamini anaweza. Kila la kheri.


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic