February 11, 2017


Washindi wa jumla wa Tuzo za wanafuzi za DStv Eutelsat Star za mwaka huu wametangazwa huku mchuano mkali ukiwa kati ya Tanzania, Ethiopia, Nigeria na Botswana.

Leoul Mesfin wa Ethiopia ameibuka mshindi wa kwanza kwenye uandishi wa Insha akifuatiwa kwa karibu na Mtanzania Davids Bwana huku kwa upande wa bango Emmanuel Ochenje wa Nijeria ndiye kinara akifuatiwa na Aobakwe Letamo wa Botswana.

Tuzo hizi ambazo zimehusisha wanafunzi zaidi ya wanafunzi 1,000 kutoka mataifa 20 barani Afrika zimeandaliwa na Multichoice Afrika kwa kushirikiana na shirika la mambo ya anga la Eutelsat na zina lengo la kukuza vipaji vya kiakili kwa watoto ili kuleta mageuzi endelevu na yenye tija katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia

Moja ya vigezo vikubwa kwa mshiriki kushinda ni kiwango cha juu cha usahihi wa alichoandika, ubunifu wa kisayansi, uhalisia wa alichokiandika na dhana ya ugunduzi aliyoijenga kwenye andiko au bango lake. Dhana ya mwaka huu imelenga kuwajengea wanafunzi mtazamo wa umuhimu wa setelaiti kwa maendeleo ya teknolojia barani Afrika.

Leoul Mesfin anapata fursa adhimu ya kufanya ziara nchini Ufaransa katika jiji maarufu la Paris na kutembelea kituo kikubwa cha anga cha Eutelsat na pia fursa ya kwenda kushuhudia  urushwaji wa setelaiti angani wakati Davids Bwana atapata fursa ya kwenda Afrika Kusini kutembelea ofisi za Multichoice pamoja na Idara ya anga ya Afrika Kusini akiwa kama mgeni maalum wa Multichoice.

Kwa upande wa washindi wa bango, nao watatembelea kituo cha Anga cah Eutelsat jijini Paris na kujifunza mambo kadhaa kuhusu uundwaji wa satellite.

Shule walikotoka washindi wote wanne zitapata zawadi ya kufungiwa ving’amuzi vya DStv pamoja na kifurushi maalum cha Elimu.

Akizungumza baada ya matokeo hayo kutangazwa mkuu wa jopo la watahini wa tuzo hizo Claudie Haigneré, mwanamama mwenye sifa na ujuzi mkubwa katika elimu ya anga na pia ameshawahi kuwa Waziri huko Ufaransa na sasa ni Mshauri maalum wa Mkurugenzi Mkuu wa  shirika la masuala ya anga la Ulaya (European Space Agency - ESA) amesema “kushiriki kwangu kwenye tuzo hizi kwa mara ya kwanza ku menipa mwangaza mwingine hususan kwakuwa mada ya mwaka huu ilikuwa yenye kutoa changamoto kubwa. 

Mitazamo na mawazo yaliyotolewa na washiriki kuhusiana na hatma ya sayansi ya setelaiti yameonyesha bayana ni jinsi gani kizazi kipya cha wanasayansi wa Afrika kilivyo na uchu na ari kubwa ya kuleta mbapinduzi makubwa katika sekta hiyo kwa manufaa ya bara la Afrika. Sisi watahini tulijikita kwenye mjadala mzito ili kuhakikisha tunamtunuku ushindi Yule hasa anayestahili.”

Akizungumza kwa Furaha kubwa juu ya matokeo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania Maharage Chande amesema wamefurahishwa sana na matokeo hayo na huu ni uthibitisho tosha kuwa watanzania wana uwezo mkubwa wa kushindana na kushinda katika anga za kimataifa. “Sisi Multichoice Tanzania tunasema Ni Zamu Yetu! Ni zamu yetu watanzania kuwika kila mahali duniani kwani uwezo huo tunao na sasa ari hiyo pia tunayo.

Kitendo cha kijana huyu kuibuka miongoni mwa washindi katika mashindano yanayohusisha kazi bora kabisa kutika mataifa 20 kote barani Afika ni heshima kubwa sana kwetu sote” alisema Maharage na kuongeza kuwa hii itawatia sana moyo wanafunzi wa Tanzania na hivyo kuongeza jitihada na bila shaka mwakani washindi wa kwanza kwa pande zote watatokea Tanzania.Pamoja na mwanamama Claudie Haigneré, Wengine walioshiriki kwenye jopo hilo la watahini ni pamoja na  Mtanzania Jenerali Ulimwengu, Msomi mwanasheria na nguli wa Habari hapa nchini; Ronke Bello, Afisa Mtendaji Mkuu wa Innovative Technology Literacy Services Ltd (Nigeria); Rodney Benn, Mkurugenzi wa Kanda (Africa) wa shirika la Eutelsat na  Melt Loubser, Meneja Mkuu wa Teknolojia ya Matangazo kutoka MultiChoice Africa. 


Wengine ni Elizabeth Ohene Muandishi wa habari ambaye aliwahi kuwa Waziri nchini Ghana; Prof. Stephen Simukanga,  aliyekua Kansela wa Chuo Kikuu cha Zambia ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Elimu ya Juu nchini Zambia  na John Ugbe, Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Nigeria.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV