March 22, 2017




Kocha Mkuu mpya wa Singida United, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, amerudi kwake Ghana huku akiacha orodha ya majina ya wachezaji anawaowahitaji ambao ni Wazimbabwe, Donald Ngoma, Thabani Kamusoko na Simon Msuva, wote kutoka Yanga.

Mholanzi huyo aliyesitishiwa mkataba na Yanga kwa kile kilichoelezwa anguko la kiuchumi, alisaini mkataba wa miaka miwili wiki iliyopita kwa ajili ya kukinoa kikosi hicho.


Kocha huyo, mara baada ya kusaini mkataba huo, alifanikisha usajili wa kiungo mchezeshaji, raia wa Zimbabwe, Tafadzwa Kutinyu kutoka Klabu ya Chicken Inn ya nchini humo.

Habari tulizozipata kutoka kwenye moja ya mitandao kutoka nje ya nchi, orodha hiyo ya wachezaji anaowahitaji, tayari ameikabidhi kwa viongozi wa Singida.


Pluijm kwenye ripoti yake, pia imempendekeza mshambuliaji aliyekuwa mfungaji bora kwenye Kombe la FA kutoka Ndanda FC ya Mtwara, Atupele Green.

“Kwenye listi ya usajili ambayo kocha wetu Pluijm ametukabidhi, imetoa mapendekezo ya wachezaji watano hadi saba wa kimataifa aliopanga kuwasajili msimu ujao wa ligi kuu.

“Kati ya hao wa kimataifa, tayari ameanza na kiungo raia wa Zimbabwe ambaye ni Kutinyu, ni chaguo la kocha, pia katika orodha hiyo, wapo wachezaji nyota na tegemeo wa Yanga ambao ni Ngoma, Kamusoko na mfungaji anayeongoza kwenye msimu huu wa ligi kuu ambaye ni Msuva.

“Pia, ametukabidhi jina la Atupele anayeichezea Ndanda FC ambaye alikuwa mfungaji bora kwenye Kombe la FA, mwaka jana, hivyo malengo yetu ni kuona tunakuwa na kikosi imara kitakacholeta changamoto ya ushindani msimu ujao wa ligi kuu,” alisema mmoja wa viongozi wa Singida.

Akizugumzia usajili wake, Pluijm alisema kitu kikubwa anachokiangalia kwenye usajili wake ni nidhamu, kujitambua na malengo ya mchezaji na siyo kitu kingine.


“Nashukuru tayari nimeanza usajili wangu kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu kwa kumsajili Kutinyu, niseme bado ninaendelea na usajili kwa ajili ya kuleta changamoto mpya kwenye ligi kuu, lakini nitasajili wachezaji wenye nidhamu na kujitambua," alisema Pluijm.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic