March 20, 2017Huenda neema imemshukia kiungo wa Azam, Himid Mao ‘Ninja’, baada ya Klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambao ni mabingwa wa Afrika, kuulizia saini yake kwa ajili ya kumuongeza kwenye kikosi chao kabla ya kuanza mikikimikiki ya ligi kuu ya nchi hiyo.

Himid amepata shavu hilo baada ya Kocha Mkuu wa Mamelodi , Pitso Musimane ambaye timu yake ilibeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita, kukoshwa na uwezo wa kiungo huyo kwenye mechi ya kirafiki baina ya timu hizo iliyopigwa jijini hapa pamoja na mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Mbabane Swallows.

Ofisa Habari wa Azam, Jaffar Idd Maganga amesema kuwa tayari wana taarifa za timu hiyo kumhitaji kiungo huyo na wao watakuwa tayari kumuachia endapo timu hiyo itawafuata kwa ajili ya mazungumzo.

“Tunazo taarifa kwamba Mamelodi wamekuwa wakimpigia hesabu kiungo wetu na nahodha msaidizi Himid Mao ila sisi tunachosubiria ni kuona wakija kwa ajili ya kuzungumza juu ya ofa ya mchezaji huyo na kama tukikubaliana basi hatuna tatizo tutawaachia.

“Kocha wao ndiye anashinikiza kwamba wamsajili Himid baada ya kuridhishwa na uwezo wake tulipokutana nao hapa Dar lakini alimfuatilia kwenye mechi yetu ya kimataifa na kuona kwamba kuna kila sababu ya kumchukua na kumuongezea kwenye kikosi chake na sisi wala hatuna haja ya kumbania endapo tu tutaafikiana kiasi tunachohitaji,” alisema Jaffar.      


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV